Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

WAMACHINGA MSITUMIWE NA WANASIASA KUVURUGA AMANI KATIKA UCHAGUZI – RC MRINDOKO


Na Daniel Gahu – Katavi.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amewasisitiza Wafanyabishara mkoani Katavi kuhakikisha wanashirikiana katika kulinda amani ya nchi na kuwataka waepuke kutumiwa vibaya na wanasiasa kwa lengo la kuvuruga amani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Msisitizo huo, ameutoa wakati wa Kongamano la Wafanyabishara lililofanyika katika ukumbi wa Idara ya Maji Manispaa ya Mpanda, likijumuisha makundi mbalimbali katika jamii, ambapo amesema wajiepushe na kubaguana na kutenganishwa kwa misingi ya ukabila, udini au jambo lolote.

“Tunasimama na kujivunia kwamba tuna amani na mshikamano wa kutosha kwa sababu sisi sote ni watanzania, chokochoko za kipindi cha uchaguzi zisiwagawe, wakataeni watu wanaoleta chokochoko hizo wote ni watanzania tunafursa sawa za kupambania maendeleo,” amesema Mrindoko.

Ameongeza kuwa, Wananchi waendelee kufanya kazi kwa bidii katika maeneo ambayo wamekuwa wakifanya kazi kwani serikali imelekeza nguvu nyingi katika uwekezaji mpana wa sekta mbalimbali ili kuinua wananchi kiuchumi.

“Niwaombe sana tunapokuwa tunaendelea kuchapa kazi tukumbuke kutunza na kulinda miundombinu ambayo serikali imewekeza ili wananchi waweze kupata huduma bora za kijamii, fichueni wale wote wenye nia ovu wanaoweza kuiharibu kwa namna yoyote ile” ameongeza Mrindoko.

Aidha amewataka wananchi wote na makundi hayo kuendelea kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 ili kuweza kupata mitaji itakayo wawezesha kujiinua kiuchumi, pia amehamasisha wananchi kushiriki uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu pamoja na kufuata sheria za uchaguzi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *