Na Saada Almasi, Itilima – Simiyu.
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imedhamiria kulipa madai ya fidia kwa Wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali kama vile ya afya, barabara, elimu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri malipo yso kutoka Serikalini .
Kauli hiyo, imetolewa na Waziri Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika ziara yake ya kikazi katika Kijiji cha Simiyu Kata ya Migato Wilayani Itilima Mkoani Simiyu, iliyolenga kusikiliza kero za ardhi kwa wananchi hao.

Katika ziara hiyo, Dkt. Akwilapo aliambatana na wawakilishi toka ofisi ya Ardhi mkoa, pamoja na Mkuu wa mkoa huo, Anamringi Macha na kusema kuwa tayari serikali imefanya mapitio ya fidia ambazo zinadaiwa na wananchi ambao wamekuwa na moyo wa kizalendo kujitoa na kupisha miradi hiyo, hivyo kuwalipa ni wajibu.
“Wizara imekaa na kuafikiana kwa maelekezo ya Rais kwamba hadi kufika mwezi Disemba mwaka huu madai ambayo wananchi wamekuwa wakitudai ambao walipisha miradi ya kimaendeleo tuwe tumesha walipa,kwanza walichofanya ni kuonyesha uzalendo lakini pia huduma hizi zinapoboreshwa hata wao pia wanakuwa wanufaika,” amesema Dkt. Akwilapo.

Hata hivyo, ametoa maelekezo kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoani humo, Denis Masami kuendelea na zoezi la upimaji wa maeneo, huku wakitenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa Hoteli za kitalii kutokana na Hifadhi pamoja na mapori mengi kuwepo ndani ya mkoa huo.
Dkt. Akwilapo amesema, “hapa mmepakana na Mbuga ya Serengeti, kuna pori la Akiba Maswa ambalo asilimia 75 limechukua eneo la wilaya ya Meatu na bado yapo mengine mengi na watalii wanakuja kwa wingi, hiyo ni fursa nzuri na kwa kiwango cha mapato yanayoingizwa na watalii yanashawishi kuendeleza vizuri sekta hiyo kwa hiyo tukipima na kuacha maeneo ya kimkakati kwa kwa ajili ya ujenzi wa hoteli kubwa za kitalii tutaingiza kipato na kuzalisha ajira nyingi kwa wazawa.”

Awali, akitoa ripoti ya mkoa mbele ya Waziri, Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amesema Halmashauri za mkoa huo zimetenga zaidi ya ekari elfu 43 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda ,biashara ,hoteli ,masoko, michezo na kilimo ambapo kati ya hizo ekari elfu 3800 zimetengwa kwa jaili ya ujenzi wa kongani za viwanda.
“Katika miaka mitano na nusu iliyopita mkoa wa Simiyu umepiga hatua kubwa za kimaendeleo ya huduma za kijamii maendeleo ambayo yanadhihirika kupitia maisha ya watu na sasa zaidi ya ekari elfu 43 zimetengwa kazi ambayo inafanyika kwa kushirikiana na wizara ya ardhi,na baadhi ya changamoto ambazo bado zipo atika sekta hizi tunaendelea kupamana nazo ili wananchi wa mkoa huu waendelee kuishi kwa tabasamu katika nchi yao,” amesema RC Macha.

Hata hivyo, Kamishna Msaidi wa Ardhi Mkoa wa Simiyu, Denis Masami ameiomba Wizara hiyo kuwapatia fedha kwa ajili ya uhuishwaji wa viwanja pamoja na upimaji wa viwanja vipya katika eneo la Izunya, ambavyo vinahitajika na watumishi kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwepo makazi, kwakuwa Simiyu inakua kwa kasi hali inayoongeza uhitaji wa maeneo hayo.
“Tumekuwa na kliniki ya ardhi kwa maelekezo ya Rais ambayo tumeifanya katika maeneo 35 ya wilaya 6 za mkoa huu na kufanikiwa kutatua migogoro 151 ya wananchi na kutoa hati miliki 723 lakini bado tuna omba fedha kwa ajili ya kuhuisha upimaji wa viwanja zaidi ya 800 ambavyo vinahitaji shilingi milioni 254, ili kukamilisha upimaji pamoja na upimaji mpya unaohitaji shilingi milioni 520 kwa ajili ya kufidia na kupima kwa maana hakuna mradi mkubwa wa viwanja ambavyo watumishi wengi wanamahitaji navyo,” alisema Denis.


