WALIMU WAADHIBUNI WATOTO KWA UPENDO MSITUMIE HASIRA – DKT MUTAHABWA

Na Pascal Tuliano – Tabora.

Walimu wa shule za msingi na sekondari nchini wameaswa kuwafundisha na kuwaonya wanafunzi kwa upendo ili kuilinda rasilimali hiyo muhimu katika taifa.

Rai hiyo imetolewa na kamishna wa elimu nchini Dkt. Lyabwene Mutahabwa wakati alipomuwakilisha katibu mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia prof. Carolyne Nombo katika Uzinduzi wa Mafunzo kwa walimu wapya wa somo la Elimu Biashara (Zamani Commerce) uliofanyika katika chuo Cha Ualimu Tabora (TTC).

Amesisitiza kuwa mtoto ni rasilimali muhimu ya nchi ambayo inapaswa kulindwa kwa hali na mali ili kujenga jamii bora ya kesho.

“Mwalimu haupaswi kumuadhibu mwanafunzi ukiwa na hasira au jazba, kufanya hivyo utajikuta unamuumiza vibaya mtoto. Wazazi wamekuamini sana kukupa mtoto wao ili umfundishe, hivyo unapaswa kuwafundisha na kuwaonya kwa upendo pale wanapokosea.”

Katika hatua nyingine, Dkt. Mutahabwa amesema serikali itaendelea kutoa mafunzo ya mtaala ulioboreshwa kwa walimu wote nchini ili kuhakikisha wanakuwa bora katika eneo la ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya elimu nchini (TET), Dkt. Aneth Komba amesema serikali imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 9.9 ili kukuza sekta ya elimu nchini kupitia eneo la mafunzo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutambua na kuunga mkono juhudi za mafunzo hayo katika kufanikisha utekelezaji wenye ufanisi katika mitaala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *