Walimu mbaroni kwa kuwafanyia mtihani wa Darasa la 7 wanafunzi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia walimu wanne kwa tuhuma za kuwafanyisha mitihani ya darasa la saba wanafunzi watatu wa sekondari katika Shule ya Msingi Igulumuki Wilaya ya Sengerema mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Septemba 22, 2023; Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amewataja walimu wanaoshikiliwa ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Sima wilayani humo na Msimamizi Mkuu wa Mitihani katika shule ya Msingi Igulumuki, Maiko Sheusi (35).

Wengine ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Kilabela ambaye ni msimamizi wa mtihani mkondo namba 2, Musa Mwashihava (38), Mwalimu wa Shule ya Sekondari Buzilasoga, Bonasi Balozi (33) na Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Msingi Igulumuki, Azizi Mohamed (36).

Mutafungwa amesema wanafunzi wanaoshikiliwa wote wana miaka 14 wanaosoma shule ya Sekondari Sima Kata ya Igukumuki wilayani humo wakidaiwa kuingizwa kwenye chumba cha mtihani kwa ajili ya kufanya mitihani hiyo kwa niaba ya wanafunzi wengine.

Amesema tukio hilo lililotokea Septemba 13, Mwaka huu, baada ya Kamati ya Mitihani ya Wilaya ya Sengerema kutembelea na kukagua namna mitihani hiyo inavyofanyika na kubaini udanganyifu huo ambapo mkondo namba mbili na namba tatu wa shule hiyo ilibainika kuwa na wanafunzi wa Sekondari wakifanya mitihani hiyo.

“Watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo baada ya upelelezi kukamilika. Tunaendelea kuimarisha ulinzi maeneo yote na hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wahalifu na wadanganyifu wa aina yoyote,” amesema kamanda huyo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *