Na Clavery Christian Bukoba – Kagera.
Wadau wa zao la Kahawa wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba, wamekutana na kujadili namna ya kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa zao hilo muhimu kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkuu wa wialaya ya Bukoba Erasto Sima alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ina mchango mkubwa katika uzalishaji wa kahawa nchini, hivyo ni muhimu kwa wadau wote kushirikiana kuboresha sekta hiyo.

Alisisitiza kuwa kikao hicho kiwe jukwaa la kubadilishana uzoefu kuhusu mafanikio, changamoto na mbinu bora za kuongeza tija katika zao la kahawa wilayani humo.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima alibainisha kuwa bei ya kahawa inategemea ubora wake, hivyo akawataka wadau kuhakikisha wakulima wanapatiwa miche bora pamoja na elimu sahihi ya utunzaji wa mashamba.

Kikao hicho kilijadili hali ya uzalishaji ambapo kwa sasa wakulima wanapata wastani wa kilo 700 hadi 1,200 kwa hekta. Wadau walikubaliana kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji ikiwemo kupanua maeneo ya kilimo na kusambaza miche bora kwa wakulima.
Hata hivyo, changamoto kadhaa zimeendelea kuikabili sekta hiyo, zikiwemo magonjwa ya mimea, wadudu waharibifu, mnyauko, kupungua kwa rutuba ya udongo, ukosefu wa mitaji pamoja na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali wa wilaya, taasisi za usalama, Tanzania Coffee Board, Kagera Cooperative Union (KCU), Tanzania Agricultural Research Institute Maruku, pamoja na wanunuzi wa kahawa.
Wadau hao wanatarajiwa kutumia mapendekezo yaliyotolewa katika kikao hicho kuweka mikakati thabiti itakayosaidia kuinua uzalishaji wa kahawa na kuongeza kipato kwa wakulima wa Wilaya ya Bukoba.



