WAKURUGENZI EPUKENI KUTENGENEZA MADENI MAPYA YA WAKANDARASI – RC MRINDOKO

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa wa Katavi kuepuka kuanzisha madeni mapya Kwa wazabuni kwakuwa Serikali hutenga fedha kamili Kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na hulipa madeni yote Kwa kutumia bajeti iliyopo pasipo kuongeza madeni mengine.

Agizo hilo amelitoa katika kikao kazi mei 22, 2025 kilicho wakutanisha mkuu wa mkoa, wazabuni na wakuu wa taasisi mbalimbali za umma, ambapo walikadili jitihada zinazofanywa na Serikali kushughulikia madeni ya wazabuni pamoja na changamoto wanazokutana nazo.

Amesema kuwa, baadhi ya watumishi wasio waaminifu wamekuwa wakichelewesha kushughulikia madai ya wazabuni hali inayosababisha mlundikano wa madeni na kusema Wazabuni wanapaswa kuzingatia matumizi sahihi ya nyaraka za zabuni ili kuepuka mganganyiko unaoweza kujitokeza wakati wa ulipaji.

“Upo mkakati wa kulipa madeni yote ya wazabuni kupitia bajeti ya kipindi Cha miaka mitatu. Tayari tumeanza kupunguza madeni tangu bajeti ya mwaka 2024/2025, na tunatarajia hadi kufikia mwaka 2026/2027 tutakuwa tumemaliza kulipa madeni yote,” amesema Mrindoko.

Ameongeza kuwa kutokana na jitihada hizo, Serikali ya mkoa imefanikiwa kupunguza jumla ya madeni ya wazabuni kutoka shilingi 2.38 bilioni hadi kufikia malipo ya shilingi milioni 755.16 Kwa baadhi ya wazabuni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Katavi, Amani Mahela ametoa wito Kwa wafanya biashara mkoa wa Katavi kujiunga katika chama Chao ili kurahisisha ufuatiliaji wa madeni pamoja na upatikanaji wa taarifa sahihi kutoka Kwa mamlaka husika.

“Taarifa nyingi kutoka serikalini huletwa katika ofisi zetu, lakini wafanya biashara wengi hawazipati kwa sababu hatuna taarifa zao sahihi hiyo nawasihi sana mjiunge kwenye chama” amesema Mahela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *