Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo amewataka wananchi kuzitumia maabara za Mamlaka kuchunguza mazao ya kilimo, ili kutambua usalama wake kabla ya matumizi.
Mkurugenzi ndiyo amesema hayo Agosti 7, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa Habari waliotembelea Banda la Mamlaka katika maonesho ya Kitaifa Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela.
Amesema, “unaweza kuwa na mazao yako kabla hujataka kuuza njoo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali tuchunguze kama ni salama kwa mlaji jambo linalomsaidia mkulima kuchukua hatua stahiki,” amesema.

Katika Hatua Nyingine, Ndiye amewataka wakulima kuhakikisha wanazingatia mbinu za kitaalamu wakati wa uvunaji wa mazao ili kuepukana na Sumukuvu.
“Wakati wa mavuno tuepukane na tabia ya kurundika mazao kwa makundi, lakini pia tuzingatie mbinu za kisasa za kuhifadhi, ili kuepukana na tatizo la Sumukuvu,” amesema Ndiye.

Kwa upande wao Wakulima toka mkoani Singida, Jackson Ibrahim na Mwiga Teka wameishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwapa Elimu ya Kukabiliana na Sumukuvu.
“Tumepata elimu nzuri, Sumukuvu inasumbua sana na sasa tumejua namna ya kuikabili, Tunaomba Mkemia Mkuu wa Serikali afike mpaka huku chini atusaidie kutuelimisha zaidi,” wamesema.


