WAKULIMA WA PAMBA MASWA WAPEWA ELIMU MIFUMO YA KIFEDHA

Na Saada Almasi, Maswa – Simiyu.

Baada ya serikali kupendekeza Wakulima wa zao la Pamba kutumia mifumo rasmi katika kupokea malipo baada ya kuuza mazao yao, Maafisa ushirika wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Wilayani Maswa mkoani Simiyu wametoa mafunzo maalum kwa Wakulima wa zao hilo juu ya namna sahihi ya kutumia mifumo hiyo, ili kuepusha dhuluma zilizokuwa zikijitokeza msimu uliopita.

Hatua hiyo inafuatia baada kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima hao kudhulumiwa na watendaji wa vyama vya ushirika (AMCOS), kwa kushawishika na kukimbia na fedha zao za malipo jambo ambalo limeifanya serikali kutoa maelekezo ya kutumia mifumo rasmi ambayo maafisa wa tume ya maendeleo kwa kuona umuhimu wake wamewaelekeza wakulima namna bora ya kutumia mifumo ya kibenki na hata mitandao ya simu ili pesa zao ziwe salama hasa kuelekea msimu wa ununuzi wa pamba mwaka 2026/2027.

Akizungumza na Wakulima katika chama cha msingi cha ushirika cha Sola wilayani humo afisa ushirika Mbaraka Maleu amewaeleza wakulima hao kuwa kitendo cha wakulima kujisajili katika mifumo rasmi kutaongeza uwazi wahatu nzima ya ununuzi bila kuacha sintofahamu.

“Hatua hii inaongeza uwazi kwamba pesa ambayo umeuza pamba yako ndiyo utakayopewa tumeona baadhi yenu msimu uliopita ulipokea pesa ambazo hazikutimia na kwa sababau ni nyingi ule muda wa kuzihesabu unaukosa badala yake unapokea pesa na kuondoka kumbe kuna kiasi ambacho mtendaji wa AMCOS amebaki nacho, tunatamani hilo lisijirudie haki yako upewe,” amesema Mbaraka.

Ameongeza, ”unapotumia mfumo wa kibenki unakuwa na uhakika pamoja na usalama wa fedha zako siku yoyote unapohitaji kutumia unauwezo wa kufanya hivyo kwa kiwango unachotaka tofauti na pale ambapo umekaa na pesa ndani ukiziangalia hata maendeleo yataonekana,” Mbaraka.

Kwa upande wake Aaron Mrema kutoka TCDC amewaeleza wakulima hao kutokuwa na hofu juu ya makato ambayo yanafanyika katika mabenki na mitandao ya simu kwani kile kinachokatwa hakilingani na pesa ambayo huwa wanadhulumiwa.

“Wapo ambao wanasema beenki wana makato makubwa niwaambie wakulima mtafunguliwa akaunti zenu ambazo zitakuwa na makato nafuu hebu fikiria unakwepa kukatwa shilingi elfu 6 katika milioni 3 pesa zikiwa benki lakini unapewa hiyo pesa mkononi ambayo haina laki moja iliyochukuliwa bila wewe kujua na mtu wa amcos ,hapo hasara ni ya nani?kwa hiyo ni bora ugharamike kidogo uokoe kingi kuliko kuamini umeokoa kumbe umeibiwa,” amesema Aaron.

Aaron ameongeza kuwa kitu cha muhimu ambacho anatakiwa kuhakikisha mkulima anakuwa nacho ni akaunti ya benki ama namba ya simu ya mtandao wake ambalo limesajiliwa na kwa jina lake kupitia utambulisho wa taifa yaani namba ya NIDA.

Wakulima wa zao la pamba mkoani Simiyu katika msimu uliopita wa 2025/2026 malalamiko yao yalitaja dhuluma kutoka kwa viongozi wa vyama wasio waaminifu,uchakachuliwaji katika mizani ya upimia pamba,na hata kuwepo kwa mnunuzi mmoja ,malalamiko ambayo tayari serikali inayafanyia kazi ili kumfanya mkulima afurahie jasho lake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *