WAKULIMA NSIMBO WALIA NA SERIKALI KUSHUKA KWA BEI YA MAZAO

Na Daniel Gahu – Katavi.

Wakulima wa Kata ya Ibindi, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi, wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na kushuka kwa bei ya mazao, hususan tumbaku na mahindi, wakisema hali hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wao na kuwatia hofu kuhusu msimu ujao wa kilimo.

Wakulima hao wametoa kilio hicho wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Wakulima Nanenane yaliyofanyika ngazi ya Wilaya katika Kata ya Ibindi, ambapo wananchi, wakulima, wataalamu wa kilimo pamoja na wadau mbalimbali walishiriki katika shughuli hiyo.

Katika sherehe hizo, wataalamu wa kilimo na lishe walitoa elimu mbalimbali kwa wananchi kuhusu mbinu bora za kilimo, uzalishaji wa mazao pamoja na umuhimu wa lishe bora kwa jamii.

Wakulima wamesema pamoja na kutumia gharama kubwa katika uzalishaji kutokana na kupanda kwa bei za pembejeo, wamejikuta wakikabiliwa na bei ndogo ya mazao yao katika soko la msimu huu wa mavuno.

Kwa mujibu wa wakulima hao, hali hiyo imekuwa ikiwafanya kushindwa kurejesha gharama walizotumia shambani, huku baadhi yao wakieleza kuwa wamepata hasara kubwa na wengine kufikia hatua ya kushindwa kujiandaa kwa msimu mwingine wa kilimo.

Mmoja wa wadau wa kilimo aliyezungumza na Jambo Media kwa sharti la kutotajwa jina amesema gharama za pembejeo zimekuwa kubwa ikilinganishwa na bei ambayo wakulima wanapata baada ya kuuza mazao yao.

“Hivi sasa mtu ili aweze kununua mfuko mmoja wa mbolea inamlazimu kuuza magunia matatu ya mahindi yenye ujazo wa kilogramu 100. Hali hii inahatarisha uwezo wa mkulima kurejea tena shambani msimu ujao wa kilimo,” amesema.

Ameongeza kuwa, licha ya Serikali kutoa ahadi kuhusu uwepo wa ruzuku kwenye mbolea, baadhi ya wakulima bado wanaona bei ya pembejeo hizo kuwa kubwa na kuwa mzigo kwao.

Ameiomba Serikali kuendelea kuwaangalia wakulima kwa jicho la huruma kwa kuweka mazingira yatakayowawezesha kupata pembejeo kwa gharama nafuu na kuuza mazao yao kwa bei inayolingana na gharama za uzalishaji.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Bibi Shamba wa Kata ya Ibindi amesema eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao mbalimbali yanayotokana na kilimo.

Amesema miongoni mwa mazao yanayozalishwa kwa wingi katika kata hiyo ni tumbaku, mahindi na mpunga, huku shughuli za kilimo zikiwa na mchango mkubwa katika uchumi wa wananchi pamoja na mapato ya Serikali.

Kutokana na nafasi kubwa ya kilimo katika maendeleo ya kata hiyo, wakulima wameeleza kuwa ni muhimu Serikali na wadau wengine kuendelea kuweka nguvu katika kutatua changamoto zinazowakabili ili kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao.

Mbali na changamoto za kilimo na masoko ya mazao, wananchi wa Ibindi wametumia fursa hiyo kueleza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Ibindi.

Wananchi wamesema kutokana na uhaba huo, wanafunzi wa shule hiyo wamelazimika kutumia baadhi ya madarasa ya Shule ya Msingi Ibindi, hali ambayo kwa mujibu wao inaathiri mazingira ya kujifunzia na inaweza kuchangia kudorora kwa taaluma.

Wameiomba Serikali na viongozi wa eneo hilo kushirikiana katika kutatua changamoto hiyo ili wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunzia.

Mgeni rasmi katika Sherehe hizo za Nanenane zilizofanyika ngazi ya Wilaya katika Kata ya Ibindi, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, ameahidi kufikisha na kushughulikia kero mbalimbali za wakulima na wananchi katika maeneo husika.

Katika hatua ya kuanza kutatua changamoto ya elimu, Mbunge huyo ameahidi kuchangia mifuko ya saruji itakayotosha kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyohitajika katika Shule ya Sekondari Ibindi.

Aidha, ameahidi kutoa shilingi milioni 10 kutoka katika Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.

Hatua hiyo imepokelewa kama sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya elimu katika kata hiyo, huku wananchi wakitarajia utekelezaji wa ahadi hiyo utasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa madarasa.

  • Wakulima walalamikia uhodhi wa mabonde yenye rutuba

Katika hatua nyingine, baadhi ya wakulima wameiomba Serikali kushughulikia changamoto ya baadhi ya watu kuhodhi maeneo makubwa ya mabonde yenye rutuba bila kuyafanyia shughuli za uzalishaji.

Wamesema hali hiyo inawanyima fursa wakulima wengine ambao wana uwezo na utayari wa kulima maeneo hayo.

Wamependekeza maeneo hayo yenye rutuba ambayo hayatumiki kwa uzalishaji yapitiwe na mamlaka husika na, pale inapobainika kuwa yamehodhiwa bila kutumika, yaweze kugawiwa kwa wananchi wenye uhitaji na wanaoweza kuyatumia kwa shughuli za kilimo.

Kwa ujumla, kilio cha wakulima wa Ibindi kinaelekezwa zaidi katika kupatikana kwa soko lenye tija kwa mazao yao, kupunguza gharama za pembejeo, pamoja na kuhakikisha rasilimali za ardhi yenye rutuba zinatumika kuongeza uzalishaji.

Wakulima wanasema bila hatua madhubuti katika maeneo hayo, juhudi zao za kuongeza uzalishaji zinaweza kutokuwa na tija kutokana na kutokuwepo kwa uwiano kati ya gharama wanazotumia kuzalisha na bei wanazopata sokoni.

Sherehe za Nanenane katika Kata ya Ibindi, hivyo, zimekuwa zaidi ya maadhimisho ya wakulima, bali pia zimekuwa jukwaa la wananchi kuwasilisha changamoto zinazowakabili na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha kilimo, elimu na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Kwa wakulima wa Ibindi, ujumbe wao kwa Serikali ni mmoja; uzalishaji uende sambamba na soko lenye tija, pembejeo nafuu na mazingira yatakayomuwezesha mkulima kunufaika na jasho lake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *