Wakulima mkoani Manyara, wametakiwa kuongeza thamani ya mazao ya mboga mboga na ile ya jamii ya mikunde kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao hayo, ili kupata masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi badala ya kuuza mazao ghafi kwa bei ya chini.
Akizungumza katika mafunzo ya kuongeza thamani ya mazao ya mboga mboga na mikunde yaliyoandaliwa na Shirika la World Vegetable Center kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Manyara pamoja na SIDO, Kaim Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Faraja Ngerageza amesema itasaidia kuongeza thamani ya mazao yanayopatikana ndani ya mkoa wa Manyara.

Kwa upande wake Mtafiti Mwandamizi wa Kitengo cha uchumi jamii kutoka Shirika la World Vegetable Center Inviolate, Dominick amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wakulima wanaotengeneza bidhaa mbali mbali kutokana na mboga mboga na mikunde
Meneja wa SIDO Mkoa wa Manyara, Abel Mapunda amewataka wananchi kufika katika shirika hilo la Kuhudumia Viwanda Vidogo, ili wajifunze ujasiriamali utakaowasaidia kuwainua kiuchumi.

Afisa Biashara wa Mkoa wa Manyara, Ally Mokiwa amesema mafunzo hayo yatawasaidia wafanyabiashara kuinua kipato chao kupitia ubunifu.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema yatawasaidia kiuchumi na kuwaongezea thamani.



