WAKANDARASI WAHIMIZWA MATUMIZI YA VIWANGO STAHIKI VYA TANZANIA

Na Ibrahim Rojala – Geita.

Wakandarasi nchini wamehimizwa kutumia viwango vya Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini pamoja na kutumia maabara za ndani ya nchi kupima ubora wa bidhaa.

Rai hiyo imetolewa Aprili 29,2026 na Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Ziwa Magharibi, Joseph Makene wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wakandarasi,Wahandisi na Watengenezaji wa Mitambo ya Uchimbaji wa Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt Samia Suhuhu Hassan,Manispaa ya Geita.

Kupitia mazungumzo hayo, Makene pia amebainisha mafanikio yaliyopatikana tangu kufunguliwa kwa ofisi ya TBS Kanda ya Ziwa Magharibi inayohudumia mikoa ya Geita,Shinyanga na Kagera kuwa ni pamoja  kuongezeka kwa idadi ya  vyeti vya ubora vilivyotolewa na shirika hilo.

Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Ziwa Magharibi, Joseph Makene.

“Ofisi hii imefunguliwa tangu mwezi wa tisa mwaka jana (2025) na katika mafanikio ambayo yamepatikana katika kipindi kifupi,ofisi hii imefanikiwa kutoa vyeti vya ubora 139,kwa maana hiyo viwanda 139 vya Mikoa ya Geita,Shinyanga na Kagera vimefanikiwa kupata vyeti vya ubora,lakini kati ya vyeti hivyo 139,vyeti 41 ni vipya kabisa,” ameeleza Makene.

Amewasisitiza wazalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini kuthibitisha ubora wa bidhaa zao na kupata leseni ya kutumia nembo ya ubora hatua ambayo itawezesha kutanua soko la  bidhaa ndani na nje ya nchi.

“Unapothibitisha ubora wa bidhaa yako unakuwa umeiongezea value,unaifanya ile bidhaa iweze kuuzika kwa urahisi sokoni,unakuwa unaifanya iweze kuingia katika masoko ya kimataifa, ya kikanda na ya kimataifa,” amesema Makene.

Katika hatua nyingine amewataka watengenezaji wa bidhaa nchini kuendelea kuzingatia ubora wakati wa utengenezaji wa bidhaa zao kwa kuzingatia viwango akibainisha kwamba kwa wanaokiuka taratibu hatua mbalimbali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuteketeza bidhaa zisizo na ubora ambazo zinaweza kuleta madhara kwa wananchi endapo wakizitumia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *