Na Daniel Gahu – Katavi.
Katika kuhakikisha juhudi za kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla, wajasiriamali wa wilaya ya Mpanda wamepewa wito wa kubadilisha mtazamo wa biashara na kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazojitokeza, badala ya kubaki katika uendeshaji wa kawaida usio na ubunifu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Mpanda, Kaimu Katibu Tawala ambaye pia ni Afisa Biashara, Viwanda na Uwekezaji Mkoa wa Katavi, Florence Chrisant amesema, mafanikio ya biashara yanategemea ubunifu, uaminifu na matumizi sahihi ya maarifa.

“Ni muhimu kwa wajasiriamali kuwa wabunifu, kutumia maarifa wanayopata kuboresha bidhaa na huduma zao, pamoja na kuzingatia uaminifu na haki za wateja ili kujenga biashara imara na endelevu.”
Chrisant amesema kuwa mazingira ya sasa ya biashara yanahitaji ushindani wa mawazo na ubunifu zaidi, akisisitiza kuwa wajasiriamali wadogo na wa kati ndio nguzo muhimu ya uchumi wa jamii.

Mafunzo hayo yamewakutanisha makundi mbalimbali yakiwemo makundi ya Baba na Mama Lishe, mafundi cherehani, mafundi seremala, vinyozi pamoja na wahudumu wa nyumba za kulala wageni, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuongeza tija na kupanua wigo wa biashara zao.
Washiriki wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewafungua macho juu ya namna bora ya kuendesha biashara kwa faida zaidi na kuongeza ushindani sokoni.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwa wajasiriamali wa wilaya ya Mpanda na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Katavi kwa ujumla.




