Waumini wa dini ya kiislamu wanaoswali katika msikiti wa Ijumaa wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza wameiomba serikali kuingilia kati mgogoro unaoendelea katika msikiti huo, kwani ni mgogoro ambao hauna maslahi kwa waumini na unaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Akizungumzia mgogoro huo mmoja wa waumini wa msikiti huo anaefahamika kwa jina la Masoud Mgasa amesema kumekua na mvutano kati ya bodi ya wadhamini dhidi ya kamati ya mpito ya usimamizi wa msikiti huo ambapo kupitia mgogoro ipo kesi ambayo inaendelea mahakamani ila wao wanaona ugomvi wao hauwezi ukawa ndio ukomo, hatma au mustakabali wa usimamizi na uendeshaji wa msikiti kwani msikiti wa ijumaa upo chini ya waumini wote waliosajiliwa.
Katika hatua nyingine Masoud pia amesema wamekua wakifuatilia mwenendo wa kesi hiyo inayoendea mahakamani na kuambiwa kua msikiti huo unamilikiwa na waumini 32 waliopo katika daftari la mwaka 1990,lakini wao wanasema mwaka 1990 msikiti wa ijumaa haukua na daftari la waumini hivyo daftari hilo sio sahihi na halitambuliwi na wakala wa usajili,ufilisi na udhamini (RITA) pamoja na Baraza la Waislam Tanzania ( BAKWATA).
Kwa upande wake Salma Mfaume ambae pia ni muumini wa msikiti huo amesema tangu mgogoro huo ulipoanza wamekuwa wakikosa mahitaji muhimu tofauti na hapo awali ambapo walikua wanapata huduma ya msaada kwa wanawake wajane ila kwa sasa huduma hiyo haipo hivyo anaiomba serikali iingilie kati suala hilo ili mgogoro huo uweze kumalizika.
Nae Suleman Maulid amesema msikiti huo si mali ya watu 32 kama inavyoelezwa bali una watu zaidi ya elfu moja hivyo sula hilo linapaswa kuangaiwa kwa maslahi ya watu wengi na sio kwa maslahi ya watu wachache.
Kutokana na uwepo wa mgogoro huo waumini hao wamesema wanataka kuona uchaguzi wa kiongozi yoyote wa msikiti huo lazima uhusishe waumini wote wa msikiti huo huku pia wakitaka uchaguzi huo uwe huru na wa haki.