Waiomba Serikali Kuwakamata Wote Waliohusika na Mauaji Kahama

Na William Bundala,Kahama

Kufuatia kifo cha utata cha mkazi wa mtaa wa Majengo kata ya Malunga Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga Bi. Gaudensia Shukuru (25) aliyeauawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali Shingoni kabla ya mwili wake kukutwa katika eneo la hifadhi ya msitu wa Mkweni katika kijiji cha Wendele,wakazi wa mtaa wa Majengo wameiomba serikali na vyombo vya dola kuchukua hatua  stahiki  kwa watu waliotekeleza mauaji hayo ili iwe fundisho kwa wengine.

Ombi hilo limetolewa leo (Mei 30,2024) wakati wakizungumza na Jambo Fm nyumbani kwa mdogo wa marehemu ulipo msiba huo mtaa wa Majengo kata ya Malunga Manispaa ya Kahama ambapo wameiomba Serikali kuwatafuta na kuwawajibisha wahususika wote waliotekeleza tukio hilo ili wananchi waache kujichukulia sheria mkononi.

Kwa upande wake mdogo wa marehemu Averina Shukuru (23) ameiambia Jambo Fm kuwa mara ya mwisho dada yake alimuaga kuwa anakwenda kuswali na hakumuona tena hadi walipokwenda polisi kutoa taarifa na kuambiwa waende mochwari kutambua miili iliyookotwa ndipo walipoukuta mwili wa marehemu dada yake.

Diwani wa Kata ya Wendele Justin Sitta ameeleza kuwa walipata taarifa ya uwepo wa mwili wa mwanamke huyo katika Msitu wa Mkweni kutoka kwa wanawake waliokwenda  kutafuta kuni na kubainisha kwamba hilo ni tukio la nane la mauaji kutekelezwa katika msitu huo na kuiomba serikali kuwaruhusu wananchi kufanya shughuli za kibinadamu ndani yake ili kukomesha vitendo hivyo

Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia aliyekuwa mume wa marehemu Jafari Magesa (31) mkazi wa mtaa wa Milambo halmashauri ya Manispaa ya Kahama,kwa tuhuma za mauaji ya mtalaka wake huyo huku chanzo kikitajwa kuwa ni mgogoro wa talaka na kugawana mali ambapo kesi ilikuwa ikiendelea mahakamani ambayo ilipaswa kuendelea kusikilizwa Mei 28,2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *