WAIOMBA SERIKALI KUFANYA JITIHADA ZA ZIADA UTOAJI ELIMU MAGONJWA YA KURITHI, YASIYOAMBUKIZA

Na Adam Msafiri, Musoma – Mara.

Baadhi ya wakazi katika Manispaa ya Musoma mkoani  Mara wameiomba serikali, mashirika ya afya na wadau kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu kuhusu magonjwa ya kurithi na yasiyoambukiza hususan selimundu (Sickle Cell), ili kuondoa mitazamo potofu inayohatarisha maisha ya wengi.

Haya yamejiri Juni 19, 2025 katika maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa selimundu Duniani (Sickle Cell) ambapo mjini Musoma,maadhimisho hayo yamefanyika katika viunga vya hospitali ya manispaa ya Musoma.

Bi Noela James mkazi wa eneo la Buhare mjini Musoma ambaye amehudhuria maadhimisho ya siku hiyo ya selimundu Duniani amesema”Mimi nimepokea maadhimisho haya vizuri kwa sababu hata mimi pia nina changamoto ya huyu mtoto,kwahiyo nimehudhuria ili nipate elimu ya namna bora ya kuishi na kumuhudumia mtoto wangu mwenye ugonjwa huu wa Sickle Cell,lakini bado jamii inahitaji elimu zaidi kuhusu magonjwa kama haya”.

Naye Bwana Malima James,Baba mwenye watoto wawili wenye changamoto ya selimundu,ametumia fursa hiyo kuishauri jamii kuhakikisha watu wanafanya vipimo kwanza kabla ya kuoana ili kubaini vinasaba vya ugonjwa huo pamoja na magonjwa mengine ya kurithi jambo litakalosaidia kutambua afya zao na kuchukua hatua za mapema za kujikinga na athari za magonjwa hayo.

Wakati huo huo Tovuti hii imezungumza na Bi Mariamu Mwita ambaye ni Muuguzi Mkunga katika hospitali ya Manispaa ya Musoma,yeye anatoa wito kwa jamii hususan kwa wazazi kusaidia kuwaibua watoto wenye dalili za selimundu na kisha kuwawahisha katika huduma za afya ili waanzishiwe matibabu haraka na kuondoa uwezekano wa madhara ya hali ya juu ya ugonjwa huo.

“Tunapochelewa kutambua hali za watoto wakiwa wachanga wakawa watu wazima wanakuja kupata changamoto ambazo ni kubwa zaidi lakini tukiwaibua mapema,tunaweza kupunguza zile changamoto zinazoweza kuwaathiri kwa mfano kupata kiharusi,changamoto ya figo pamoja na upungufu mkubwa wa damu’’Ameeleza Bi Mariamu Mwita.

Kwa upande wake Daktari wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka hospitali ya Manispaa ya Musoma Dkt Paschal Francis,akiongea kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo,ameeleza kuwa kwa sasa wanayo dhamira ya dhati ya kuielimisha jamii kikamilifu kuhusu ugonjwa wa selimundu,magonjwa ya kurithi pamoja na yasiyoambukiza ambapo wataifikia jamii kupitia njia mbalimbali ikiwemo mikusanyiko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *