WAHUSIKA MAUAJI YA MUME NA MKEWE KILIMANJARO WASAKWA


Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawasaka watu waliohusika katika mauaji ya watu wawili ambao ni mke na mume Geofrey Anael Mota (60) aliyeuawa kwa kukatwa na kitu chenye makali shingoni na mkewe Blandina Felix Ngowi (53)
ambaye mwili wake haujakutwa na majeraha.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa hii leo Mei 30, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, imeeleza kuwa watu hao waliuawa wakiwa nyumbani kwao Mtaa wa
Msufini, Kata ya Msaranga, Wilaya ya Moshi Manispaa, Mei 29, 2025 majira ya
saa moja na nusu usiku.

“Tukio hilo limetokea ndani ya nyumba ya kupanga waliyokuwa wakiishi wanandoa hao
pamoja na kijana wao wa kiume (jina limehifadhiwa) ambaye ametoweka baada ya
mauaji hayo kutokea. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo na kuwakamata wote waliohusika na mauaji hayo,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, imearifiwa na Jeshi hilo kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya rufaa KCMC Moshi kwa uchunguzi na taratibu zingine, huku likitoa wito kwa Wananchi kutoa ushirikiano pamoja na taarifa zitakazowezesha kuwapata waliohusika na tukio hilo, ili hatua za
kisheria ziweze kuchukuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *