WAHIMIZWA USHIRIKIANO KUTAMBUA, KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANAWAKE NA WATOTO

Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) mkoani Mwanza wametakiwa kushirikiana kwa karibu na serikali katika kutambua na kutatua changamoto zinazokabili makundi hayo ili kuwaondoa kwenye vitendo vya ukatili.

Wito huo umetolewa leo Agosti 13, 2025 wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya siku tatu ya Kamati ya Mkoa ya kupinga na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto NPA-VAWC 2024/25–2028/29 II, ambapo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana, alisema kila mjumbe anapaswa kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kubaini matatizo yanayowakwamisha kushiriki katika maendeleo ya uchumi na kuyaondoa.

“Ukatili kwa wanawake na watoto unazuia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla, kwani serikali inalazimika kushughulikia majeraha ya ukatili kama vile matibabu na ushauri nasaha. Hivyo, wajumbe nawaomba mkatekeleze wajibu wenu,” alisema Balandya.

Katika hatua nyingine Balandya amesema kuwa mchanganyiko wa wajumbe kutoka taasisi na madhehebu mbalimbali ya dini unalenga kufikia makundi yote ya jamii na kuhakikisha elimu ya kupinga ukatili inawafikia wote.

Akizungumzia changamoto ya watoto wanaoishi mitaani, Balandya amesema kila kiongozi katika eneo lake ahakikishe anafikisha ujumbe kwamba si sahihi kuwahudumia watoto wanaoomba pesa mitaani, kwa kuwa kitendo hicho kinaendeleza tatizo hilo.

Akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Gabriel Mashauri, amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wajumbe kupitia maeneo manane ya afua zinazopaswa kufuatwa, na baada ya siku tatu kila mmoja atakuwa na ufahamu wa majukumu yake ya kila siku katika kuhakikisha watoto na wanawake wanalindwa dhidi ya ukatili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *