Wahamiaji wasiohamishika 3,319 ambao wameishi nchini kwa zaidi ya miaka 50 wakiwa na asili ya mataifa jirani ya Burundi, Comoro, Msumbiji na Rwanda, wamekabidhiwa vyeti vya uraia wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi.
Rais Dk.Mwinyi amewakabidhi vyeti hivyo leo tarehe 05 Septemba 2023 katika hafla iliyofanyika Ikulu, Zanzibar, ambapo amesema nchi imeandika historia na kufurahi kutekeleza ahadi yake aliyoitoa baada ya kuingia madarakani mwaka 2020.
Rais Dk.Mwinyi ametoa wito kwa Idara ya Uhamiaji nchini kuziimarisha sheria zilizopo hususani sheria ya uraia wa Tanzania kwa kuwa sheria hii haijafanyiwa mapitio kwa kipindi kirefu kwa madhumuni ya kuiwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowahusu wananchi na wageni.