
Wagonjwa wamekwama kupata matibabu katika hospitali mbalimbali nchini Kenya kufuatia mgomo wa madaktari unaolenga kuwezesha utekelezaji wa mahitaji ya nafasi za lazima za mafunzo ya utabibu kwa zaidi ya madaktari waliohitimu 4,000.
Madktari hao walioanza mgomo siku ya Alhamisi, pia wanadai kurejeshewa ushuru wa nyumba uliokatwa katika mishahara yao, kucheleweshwa kulipwa mishahara na kushindwa kuwasilisha makato ya kisheria pamoja na utekelezaji wa mfumo wa bima ya afya na kuwahakikishia madaktari wanaotoa huduma chini ya mpango wa afya kwa wote kuajiriwa kama ilivyokubaliwa katika makubaliano ya pamoja ya 2017.
Mbali na serikali kusema haina bajeti ya kutekeleza masharti hayo, mahakama Jumatano, ilisitisha mgomo huo, na kuwataka madaktari na serikali kufanya mazungumzo ya kufuta utata uliopo kwa haraka, kupitia mazungumzo yenye tija.
Kufuatia mgomo huo siku ya Alhamisi, wagonjwa walishindwa kupata matibabu kutoka katika vituo cha afya vya umma na kulazimika kutafuta huduma hizo kwenye zahanati binafsi.

Baadhi ya hospitali ambazo hazikuathirika na mgomo huo, zilipokea viwango vya chini vya huduma za afya, baada ya madaktari kususia kazi kama ilivyoshuhudiwa mjini Mombasa.
Kwa muda sasa utekelezaji wa mkataba wa makubaliano wa 2017-2021 ulioazimia kutatua uhaba wa madaktari, kuweka nyongeza ya mishahara na kuimarisha mazingira ya kazi, kuwapandisha madaktari vyeo na kupatikana kwa vifaa hitajika vya matibabu, na utekelezaji wa mfumo wa bima ya afya umesababisha zogo hili kutokana na kigugumizi cha serikali kuutekeleza.