Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Morogoro, ACP Samweli Kijanga amewatahadharisha wafugaji wanaokiuka sheria kwa kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima kwa makusudi na kuwadhuru kwa kutumia ushawishi wa kiuchumi.
Akizungumza katika vijiji vya Kunke na Makwalu, Kata ya Mtibwa, Wilaya ya Mvomero, ACP Kijanga alisisitiza kuwa vitendo hivyo ni vya kikatili na havivumiliki.

Awali, Mrakibu wa Polisi Yahaya Chande aliyeambatana naye, amewataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi pindi migogoro inapotokea, badala yake wawasiliane na viongozi wa serikali au Polisi.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Polisi Kata ya Mtibwa, Silija, amewahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa mapema wanapohisi dalili za migogoro au uhalifu.


