WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUWATAPELI WASTAAFU

Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka 49 ikiwemo kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha Sh. 5,000,000 walizojipatia kwa njia za udanganyifu.

Washitakiwa hao ni Eradius Rwechungura (43) maarufu ‘Rwamakala’, Heri Kabaju (37) maarufu ‘Babylon’, Abdurahim Karugila(42) maarufu ‘Obra’ na Eradius Apornary (22) na walidaiwa kujiwasilisha kuwa ni Maofisa kutoka sehemu mbalimbali na kujipatia fedha huku wakijua si kweli.

Wote kwa pamoja walifikishwa Mahakamani hapo Januari 31, 2025 na kusomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nura Manja mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Akisoma hati ya mashitaka, Wakili Manja alidai washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 49, moja likiwa ni la Kuongoza genge la uhalifu, 11 ya kujiwasilisha kwa utambulisho wa mtu mwingine, 13 ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine na, 23 ya kujipatia fedha kwa njia za udangifu na moja la utakatishaji fedha.

Wakili Manja alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kesi kutajwa, ambapo Washitakiwa walirudishwa ramande na shauri hilo liliahirishwa hadi Februari 14, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *