Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza, ACP Lwelwe Mpina amewataka wafanyabiashara wa miamala ya kifedha kuhakikisha wanafunga taa za kutosha na kamera za ulinzi (CCTV) kwenye maeneo yao ya kazi ili kuimarisha usalama na kuzuia matukio ya kihalifu.
Akizungumza leo Septemba 19, 2025 katika ziara yake ya kuelimisha wafanyabiashara wa Kata za Mkolani, Nyegezi, Nyashishi na Usagara mkoani humo, ACP Mpina amesema CCTV ni nyenzo muhimu ya kisasa yenye uwezo wa kusaidia kufuatilia tukio kabla, wakati na baada ya uhalifu.

Amesema hatua hiyo inapaswa kwenda sambamba na kujenga mahusiano mazuri na majirani, kutumia walinzi wa kampuni binafsi wenye sifa na mafunzo ya kisheria pamoja na kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na vituo vya polisi na viongozi wa serikali za mitaa.
“Usalama wa biashara ni jukumu la kila mmoja. Ni muhimu wafanyabiashara wakatunza kumbukumbu za wateja na wageni wanaotia mashaka, ili kuzuia vitendo vya kihalifu,” amesema ACP Mpina.

Kwa upande wao, wafanyabiashara waliopokea elimu hiyo wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuwafikia moja kwa moja na kutoa mwongozo huo, huku wakiahidi ushirikiano wa karibu katika kuimarisha ulinzi wa biashara zao.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesisitiza kuwa mapambano dhidi ya uhalifu yanahitaji mshirikiano wa wananchi wote kwa kutoa taarifa mapema na kushirikiana na vyombo vya usalama.