WAFANYABIASHARA TABORA WALIA NA USAFI MACHINGA COMPLEX

Na Pascal Tuliano – Tabora.

Wafanyabiashara katika soko la Machinga complex mjini Tabora wameulalamikia uongozi kwa kushindwa kuweka mazingira rafiki yanayohakikusha hali nzuri ya usafi pamoja na tahadhari dhidi ya majanga ya moto katika soko hilo.

Wafanyabiashara hao wamezungumza na jambo Fm na kueleza kuwa  jukumu la ukusanyaji wa taka limesahaulika jambo linasananisha hali ya uchafu katika baadhi ya maeneo huku vifaa vya tahadhari ya moto vikiwa pia ni kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara hao.

“Kwakweli hali ya usafi hairidhishi tofauti na kipindi cha nyuma ambapo watu wa taka walikuwa wanapita Kila mwezi kukusanya takataka, lakini kwa sasa hatuwaoni kabisa kwenye hili soko. Tahadhari ya moto pia hatuoni mikakati ya uongozi zaidi ni sisi wenyewe Kila mtu binafsi na eneo lake.” Amesema bi. Leah Onesmo ambaye ni Machinga katika soko hilo.

“Kwakweli mambo ya moto hapa Kila mtu anajijua na tahadhari anayoichukua lakini ukitokea moto mkubwa hapa hakuna juhudi zozote ambazo tunaona zimewekwa kama tahadhari, lakini mambo ya usafi ndo kama hivyo unavyoona mazingira haya viongozi wamejisahau kabisa.” Amesema Mathew Ijengo ambaye ni mfanyabishara.

Jambo Fm imemtafuta muweke hazina wa soko hilo ambaye amezungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa soko la Machinga Complex Tabora, anasema wao kama uongozi wa soko umewasiliana na ngazi husika zinazohusika na usafi katika soko hilo lakini jitihada zao hazijafua dafu.

“Tumejaribu kuwasiliana na uongozi kutoka manispaa lakini kila tukiwapigia simu wanaahidi kufika na hatuwaoni, zaidi tumeendelea kuwasisitiza wafanyabiashara kila mtu sehemu yake ahakikishe usafi unaimarishwa na usalama wa mali zake kwa majanga kama moto.” Amesema Muweka hazina wa soko, ndugu Spirian Mushi.

Jambo Fm imefanya jitihada za kuwasiliana na afisa biashara wa mkoa wa Tabora ili kulipatia ufumbuzi suala hili lakini jitihada hazikuzaa matunda kwa simu haikupokelewa.

Lakini malengo ya uongozi wa manispaa Tabora kwa sasa kuhakikisha mradi wa kimkakati wa soko jipya la kisasa linakamilika kwa wakati ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara hao kama anavyoeleza Ndugu Elias Mawago Kayandabila ambaye ni Mkurugenzi wa manispaa ya Tabora.

“Mradi huu wa uboreshaji wa soko unagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 19.9, ni fedha ambazo zimetengwa na serikali ili kuhakikisha wafanyabiashara hawa wanafanya kazi katika mazingira bora zaidi ya mwanzo.” Amesema Kayandabila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *