WAFANYABIASHARA MUSOMA WALALAMIKIA ONGEZEKO LA KODI YA VIBANDA

Na Adam Msafiri, Musoma – Mara.

Wafanyabiashara katika Soko kuu la Manispaa ya Musoma mkoani Mara,wameonyesha kutoridhishwa na uamuzi wa halmashauri ya manispaa hiyo wa kupandisha kodi ya vibanda kutoka shilingi 25,000 hadi 50,000 kwa mwezi,huku ada ya matumizi ya meza ikipanda kutoka shilingi 5,000 hadi 15,000.

Wakizungumza Julai 25,2025 wamesema kuwa uamuzi huo umefanywa bila wao kushirikishwa,jambo walilolieleza kuwa ni kinyume na haki yao ya msingi ya kushiriki katika maamuzi yanayowahusu moja kwa moja.

Miongoni mwa waliotoa malalamiko ni Lucy Sindika, Magesa Nyambeba na Paulo Nyakulimba ambao mbele ya Maafisa wa Manispaa, wakieleza kuwa hali ya biashara kwa sasa ni ngumu na ongezeko hilo linawapa wakati mgumu zaidi.

“Kwanza biashara sasa hivi ni hamna,ushuru kutoka elfu 5 meza mpaka elfu 25,Duka kutoka elfu 25 mpaka elfu 50 hilo ni ongezeko kubwa sana ambalo halijawahi kutokea kwa mfanyabiashara,sisi ni wajasiriamali kwanza tunapewa hela za Rais Samia za mkopo tunatakiwa turejeshe,sasa wanavyopandisha hivyo sisi tunapata nini,tunaomba waliangalie upya” amesema Mfanyabiashara Lucy Sindika.

Kwa upande wake Magesa Nyambela amesema, ”Lakini leo naambiwa kwamba kodi imepandishwa nilikuwa nalipa elfu 25 sasa naambiwa nilipe elfu 50,Mkurugenzi hajanipa barua maana mimi naelewa mpangaji lazima upewe Notice panapokuwa na mabadiliko yoyote,namwambia Rais wetu Mama Samia kwamba wafanyabiashara tunaonewa.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Soko Kuu la Musoma, Shaban Saasita na Katibu wake Sospeter Masunga,wamesema kuwa kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa walijaribu kuomba kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa, ili kujadili mustakabali wa wafanyabiashara,lakini juhudi hizo hazikufua dafu.

Akijibu malalamiko hayo, Mwanasheria wa Manispaa ya Musoma, Ediga Nditi alisema marekebisho ya viwango vya kodi yametekelezwa kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu mapato ya Halmashauri.

“Siku za nyuma kulikuwa kama kuna ofa tu ya ulipaji kwa bei hizo mlizokuwa mkilipa,lakini kutokana na hali iliyopo na namna ambavyo tulikuwa tukiendesha masoko yetu kwa sasa kumekuwa kuna hoja zinazotoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG)ambazo zinauliza ni kwa nini tunaendelea kutoza kiwango ambacho ni kinyume na sheria na mwongozo uliopo,” amesema Nditi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *