WAFAHAMU WALIOPITA KURA ZA MAONI UBUNGE VITI MAALUM MKOA WA SHINYANGA.

NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA 

 Mkutano Mkuu Maalum wa uchaguzi wa wagombea wa Ubunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Mkoa wa Shinyanga umefanyika kwa mafanikio makubwa leo katika ukumbi wa Shule ya Wasichana Shinyanga, ukishuhudia wagombea wawili wakiongoza kwa kishindo.

Katika mchakato huo uliovuta hisia za wanachama wengi, wajumbe 1,036 kutoka Wilaya za Shinyanga Mjini (133), Kahama (440), na Kishapu (227) wamepiga kura kuwachagua Wagombea wawili katika kundi la wanawake  kati ya wagombea wanane waliotia nia kugombea nafasi za uwakilishi katika bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania.

Santiel Erick Kirumba ameibuka kinara kwa kura 730, akifuatiwa kwa karibu na Dkt. Christina Christopher Mnzava aliyepata kura 719, na hivyo kufanikiwa kuibuka washindi wa nafasi hizo mbili muhimu kwa Mkoa wa Shinyanga.

Katika mchuano huo uliokuwa na mvutano mkubwa wa kisiasa, wagombea wengine waliojitokeza lakini hawakufanikiwa kuingia nafasi mbili za juu ni pamoja na Salome Wycliffe Makamba aliyepata kura 216 na Mwanahamis Munkunda aliyepata kura 196.

Wengine ni Felister Wilson Buzuka aliyepata kura 34, Alice Salvatory Kyanila (kura 29), Christina Kija Gule (kura 23) na Queenelizabeth William Makune aliyepata kura 19.

Kwa ushindi huo wa kura za maoni, Santiel Kirumba na Dkt. Christina Mnzava ni washindi katika uchaguzi huo nafasi ya Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga.

Naye msimamizi wa uchaguzi huo, ambaye ni mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego  kabla ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi huo  aliwaasa wagombea pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu kushiriki zoezi hilo kwa Amani na utulivu na kwamba katika chama hicho hakuna kushindwa wala kushinda bali ni mchakato wa kukabidhiana vijiti huku akiwataka ambao kura hazijatosha kuwa watulivu

Awali akitoa salamu za chama katibu wa mkoa wa chama cha mapinduzi ambaye pia ni  mkurugenzi wa uchaguzi Odilia Batimayao amewataka wagombea wa nafasi hizo kuwa watulivu na kutokutambiana kati ya walioshindwa na watakaoshinda kwani michakato ya chama hicho bado inaendelea hivyo kura hizo si kwisho wa maamuzi .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *