Na Daniel Gahu – Katavi.
Katika kuhakikisha Vitendo viovu vya kutoa na kupokea Rushwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba 2025, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi, wametoa mafunzo kwa Viongozi wa Dini pamoja na wa Kimila Mkoani humo kwa lengo la kuwawezesha kutoa elimu elekezi kwa waumini wao.
Mafunzo hayo yameongozwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Florence Chrisant, ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi na kuwataka viongozi hao kutumia madhabahu kutoa elimu na kukemea vitendo viovu vya rushwa na kusisitiza umuhimu wa kuhubiri amani na kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi waonapo viashiria vya uvunjifu wa sheria.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Kamanda Msaidizi wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Stuart Kiondo amesema Viongozi wa Dini wanao ushawishi mkubwa, hivyo inawapasa kwa kuaminika kwao wapaze sauti kwa kukemea maadili potofu na kuhimiza maadili mema katika jamii.
Kwa upande wake Mchungaji na Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Jimbo la Katavi ameipongeza TAKUKURU kuwaletea elimu hiyo kwa wakati, huku akiahidi kuufikisha ujumbe huo bila kusita kwa waumini wake.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu amewataka waumini wote wa Dini ya Kiislam Mkoa, kuacha mara moja tabia mbaya ya kutoa na kupokea Rushwa kwani haikubaliki hata Kwa Muumba wao.
Awali, Mchunguzi Msaidizi wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Leonard Minja, amesema kwasasa vitendo vya kutoa na kupokea rushwa mtaani vimeshamiri, ila kupitia makatazo ya Viongozi wa Dini watu watapata hofu ya kutenda vitendo viovu vilivyo kinyume na taratibu za nchi na Mbinguni kwa kusikia sauti ya Mungu.



