Ikiwa leo ni siku ya mwisho ya kujadiliwa kwa bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) baadhi ya Wananchi mkoani Dodoma wamejitokeza kutoa maoni yao kuhusu bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yenye kiasi cha shilingi bilioni 11.7.
Akizunguzmia bajaeti hiyo mkazi wa Dodoma, Maria Julias ambaye pia ni fundi cherehani amesema kuwa anatamani bajeti ya TAMISEMI ilenge zaidi kwenye TEHAMA ambapo itawarahisishia wafanyabiashara kwani dunia ipo kiganjani hivyo inawarahisishia wafanyabiashara kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii.

“Mfano mimi nikishona nguo zangu huwa naweka kwenye mitandao ya kijamii kwahiyo natumai tamisemi itatusaidia kwa upande huo”amesema Maria
Kwa upande wake, Emmanuel Mabalwe amesema kuwa amefuatilia Bunge na kuona bajeti ya Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 iliyowasilishwa na Waziri wa TAMISEMI, Mohammed Mchengerwa.

Amesema kuwa bajeti ya mwaka huu ya Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 imekuwa na ongezeko kwa kiasi kikubwa kutoka bajeti ya mwaka jana 2024/2025 ambayo ilikuwa ya tril.10.1 hadi kiasi cha tril 11.7
“Kwahiyo ongezeko ni kubwa ambapo Trilioni 1.66 ndiyo ambayo imeongezeka kwa mwaka huu na hiki ni kiwango kikubwa ambacho kitaenda kuhudumia watanzania,” amesema.

Naye Manoa Samweli amesema bajeti ya TAMISEMI ijikite kwenye masuala ya michezo kwani mpaka sasa michezo imekuwa ajira kwa vijana wengi ambao wana kipaji.
Amesema, mchezo wa mpira wa miguu unazidi kukua hivyo inatakiwa kuwepo na maboresho zaidi hasa kwenye miundombinu ya michezo kama vile viwanja jambo litakalosaidia kuweka ajira na kupata ajira kwa vijana ambao wana vipaji vya mpira.