WADAU WAGUSIA USHIRIKI WA  WANAWAKE KATIKA SEKTA YA MADINI

Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania Katika Sekta ya Madini, limefanyika chini ya Wizara ya Madini, likiwakutanisha wadau mbalimbali kujadili namna ya kuongeza ushiriki wa Watanzania hasa Wanawake na Vijana.

Jukwaa hilo limebeba kauli mbiuisemayo, “Kutoka Majadiliano Hadi Utekelezaji: Kwa Sekta Imara ya Madini kupitia Ushirikishwaji wa Watanzania na Uwajenzi wa Viwanda.”

Wakizungumza kwenye jukwaa hilo, baadhi ya wadau wamesema ushiriki wa kina mama bado hauridhishi licha ya kuwa sekta ya madini inatoa fursa kubwa.

Mmoja wa Wadau hao Mecktilder Meshack amesema takwimu zinaonesha kuwa kwenye uchimbaji wa madogo madogo ASM wanawake ni asilimia 40 hadi 50, lakini wengi wako kwenye kazi za kuchuja, kubeba na kuuza.

Amesema katika kampuni kubwa, Wanawake ni chini ya asilimia 15, idadi inayopungua zaidi kwenye nafasi za uongozi na ufundi, huku Edwin Godwin akibainisha kuwa vikwazo vikuu vinavyowazuia wanawake ni upatikanaji wa mtaji kwani wengi wao hawana dhamana ya ardhi.

Aidha, amesema kuna upungufu wa elimu ya kiufundi, vikwazo vya kitamaduni vinavyodai madini ni kazi ya wanaume na ukosefu wa ujuzi wa sheria, leseni na masoko ya kimataifa. Hali hiyo inafanya wanawake wengi kubaki kwenye mnyororo wa chini wa thamani.

Serikali kupitia Wizara ya Madini imesema inaendelea kutekeleza mikakati ikiwemo Mfuko wa Wachimbaji Wadogo, kutoa mafunzo ya thamani ongezeko na kutoa vipaumbele kwa vikundi vya wanawake.

Sheria ya Madini ya 2017 inasisitiza ushiriki wa Watanzania wote. Vikundi kama Umoja wa Wanawake Wachimbaji Tanzania navyo vimesifiwa kwa kutoa elimu na msaada kwa wanachama wake.

Hata hivyo, Wadau hao wamesisitiza kuwa ili kufikia malengo ya jukwaa hili, serikali na wadau wengine wanatakiwa kutoa mikopo nafuu, kuanzisha vituo vya mafunzo ya kiufundi kwa wanawake, na kubadilisha mitazamo ya jamii.

Kwa upande wao Wanawake wameswma wakishirikishwa kikamilifu na kuingia kwenye thamani ongezeko kama kukata vito na polishing, sekta ya madini itakuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *