Na Ibrahim Rojala – Geita.
Wachimbaji wa madini ya dhahabu mkoani Geita wametakiwa kujiepusha na vitendo vya utoroshaji wa madini kutokana na mchango mkubwa wa rasilimali hiyo kwa taifa ikielezwa kwamba watakaobainika kujihusha na vitendo hivyo watafilisiwa.
Agizo hilo limetolewa April 16,2026 na Katibu Tawala Msaidizi, Mkoa wa Geita ayeshughulikia Masuala ya Utumishi na Utawala,Herman Matemu wakati alipomuwakilisha mkuu wa mkoa wa Geita katika semina ya Elimu Sahihi ya Fedha kwa Wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini mkoani Geita yaliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Ameeleza kwamba mkoa wa Geita utaendelea kuimarisha kaguzi za shughuli za madini ili kuhakikisha sheria ya madini sura Na.123 na kanuni zake zinatekelezwa ipasavyo ili kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la mkoa na Taifa, kuunganisha wachimbaji wadogo wenye mahitaji ya utafiti za kijiolojia katika maeneo ya leseni zao ili kuweza kufanyiwa utafiti kwa gharama nafuu na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
‘Tulikuwa tunasikia zamani kwamba ukipata fedha ya madini inapotea bila habari,nadhani sasa hiyo dhana inaendelea kubadilika kutokana na elimu mbalimbali ambazo zinatolewa na wataalamu wetu na kipindi cha nyuma nilikuwa ninasikia kutoka kwa kiongozi wangu hapa, mkuu wa mkoa mstaafu kwamba Geita ilikuwa imegeuka kuwa shamba la bibi, watu wanachuma, wanaponda starehe, wanaondoka zao, lakini kwasasa Geita inapendeza,” amesema.

Akizungumza kuhusiana na lengo la semina hiyo, Mchambuzi wa masuala ya Fedha Kutoka Benki Kuu ya Tanzania,Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Kifedha, CPA Michael Israel Mwaituka amesema wamelenga kufikisha uelewa wa huduma za fedha ikijumuisha usimamizi wa fedha binafsi, ulinzi wa fedha, huduma zinazotolewa na BOT kwa niaba ya serikali zilizo na manufaa kwa wachimbaji wadogo na wa kati ikiwemo matumizi ya fursa za mikopo inayoweza kuwaongezea nguvu za uendeshaji wa shughuli zao.
‘Lakini pia uwepo wetu hapa leo ni kuja kuwasikiliza wachimbaji lakini pia kuwaeleza wachimbaji juu ya uwepo wa Programu maalum ya ununuzi wa dhahabu nchini ambayo Programu hii pia inafanywa na benki kuu ya Tanzania, tunasema ‘Domestic Gold Purchase Program, kwahiyo tunaendelea kuwasisitiza wachimbaji wadogo na wa kati kuweza kujinufaisha wao kwa kutumia soko hili la dhahabu ambalo ni la nchini kupitia Benki kuu ya Tanzania’ameeleza CPA Michael

Nae, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel ameleeza kuhusu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya madini mkoani Geita ikiwa ni pamoja na uwepo wa soko la kwanza la madini kuwahi kuanzishwa nchini madini lililo na leseni zaidi ya 100 ikilinganishwa na leseni mbili pekee zilizokuwepo wakati wa uanzishwaji wa soko hilo mnamo mwaka 2019.
Kupitia Semina hiyo,6Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Madini, Mkoa wa Geita (GEREMA), Titus Charles Kaguo ameeleza kwamba wachimbaji wako tayari na wanajitahidi kutafuta fedha kupitia madini akidokeza kwamba endapo wataielewa elimu waliyopatiwa itasaidia ongezeko la mapato kupitia sekta hiyo na kuiomba BOT kupitia mchakato wa ununuzi wa dhahabu kuyakumbuka makundi yote yaliyo katika mnyororo wa thamani wa madini ya dhahabu ndani ya mkoa wa Geita.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Wanawake Wachimbaji wa Madini ya Dhahabu Mkoa wa Geita (GEWOMA), Asia Hussein ametumia semina hiyo kuiomba serikali kufanya ukarabati wa barabara za migodini.
‘Sisi tunatoa pesa nyingi sana halmashauri,na halmashauri tunakopeleka pesa lakini bado miundombinu yetu ya barabara sio rafiki,kwahiyo tukuombe kama wachimbaji, ukienda Matabe barabara ni nyingi, ukienda Ushirombo barabara hazipitiki,ukienda Lwamgasa barabara hazipitiki,tunawaomba kwa heshima na taadhima mtusaidie masuala ya barabara,” amesema Asia.

Joseph Nehemia na Bi.Hapiness Cosmas ambao baadhi ya wachimbaji waliohudhuria semina hiyo wameeleza kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni kutokuwa na uelewa wa utunzaji wa taarifa za fedha zinazohusisha mapato na matumizi yatokanayo na kazi ya uchimbaji wa dhahabu kuhusisha matumizi mengi ya fedha ambayo mara nyingi huwa hayatabiriki.



