
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amewataka waandishi wa habari kutumia ipasavyo kalamu zao ili kulinda amani ya nchi.
Msigwa ametoa kauli hiyo leo Disemba 13,2024 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhiwa ofisi kutoka iliyokuwa Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Nawashukuru sana waandishi wa habari wenzangu kwa namna mnavyofanya kazi yenu ya habari kwa nguvu na weledi, naomba tuendelee kushirikiana, naamini tutafanya kazi kwa kukidhi matumaini na matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ametupa nafasi ya kulitumikia taifa,”amesema.
Msigwa pia ametumia wasaa huo kuelezea baadhi ya miradi inayoendelea katika Wizara hiyo kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kutoa wito kwa waandishi wa habari kuendelea kushiriki katika kutangaza miradi hiyo ili Watanzania wajue kazi inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
Pia amewapongeza viongozi wanaoondoka na kumuachia kijiti kwa kazi kubwa waliyoifanya, ndani ya idara hiyo kwani alivyoiacha ni tofauti na na alivyoikuta huku akiahidi kuwa watasonga mbele zaidi.
Kwa upande wake aliyekuwa Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya HABARI-MAELEZO Balozi Tobias Makoba amewapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kujitoa katika kuelimisha jamii ya watanzania na kuongeza kuwa katika kipindi chote alichofanya nao kazi ameona uzalendo ndani yao.
“Nawashukuru sana waandishi wa habari kwa kipindi tulichofanya kazi pamoja na kwa ushirikiano, mmekuwa wazalendo katika utekelezaji wa majukumu yenu, nikitolea mfano wa namna tulivyokesha pamoja kwenye tukio la ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo,”amesema.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Mkapa ametoa shukrani kwa viongozi na wafanyakazi wa Idara ya Habari – MAELEZO kwa kufanya kazi kwa ushirikiano katika ujenzi wa Taifa katika kipindi chote walichokuwa pamoja.
“Tunaikabidhi Idara ya Habari – MAELEZO kutoka iliyokuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambayo sasa ni Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa na Taasisi zake tatu ambazo ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), na Bodi ya Ithibati,”- Mkapa.


