Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama ngazi ya Kata na Wilaya Wilayani Magu Mkoani Mwanza, wametakiwa kufanya kazi kwa weledi huku zikizingatia suala la kutunza siri za watoa taarifa ili kuepusha chuki na uhasama katika jamii.
Rai hiyo imetolewa na Mkufunzi wa Elimu ya Uraia na Utawala Bora kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, ASP Iddah John Ringo wakati akitoa mafunzo kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na Usalama ngazi ya Wilaya na Watendaji wa Kata Wilayani Magu.
Amesema, Wakuu hao wa vyombo vya ulinzi ni watu muhimu sana katika jamii na wamekua wakipokea taarifa nyingi za siri katika maeneo yao hivyo pale wanapopokea taarifa hizo wanatakiwa kuzitunza ili kuwalinda watoa taarifa.

“Tunawaomba wakuu wa vyombo na watendaji wa kata wanavyopewa zile taarifa basi mafriji yao yagandishe wawe na tabia ya kuwalinda wasiri wao wasitoe taarifa ya wasiri wao kwa sababu kwanza wanatengeneza uhasama wa mtoa taarifa na mashtakiwa au mtuhumiwa,” alisema Ringo.
“Na hii inasababisha wale wenye nia nzuri ya kutoa taarifa zitakazosaidia kupambana na majanga ya kihalifu kukaa kimya na kusababisha suala dogo kugundulika likiwa kubwa hali itakayopelekea Serikali kutumia gharama au nguvu kubwa lakini kumbe wangepata taarifa za mwanzo wangezibiti mapema,” aliongeza.
Katika hatua nyingine ASP Ringo amewataka wakuu hao wa vyombo vya usalama kuhakikisha wanashiriki katika matukio au shughuli za kijamii ili kunasa taarifa za uhalifu na wahalifu kabla au baada ya kutokea kupitia minong’ono au mazungumzo ya wananchi.

“Watendaji wa kata wajue wanawajibu wa kushiriki katika matukio na shughuli mbalimbali za kijamii ili kujiweka karibu na watu lakini pia yatamsaidia kupata taarifa ambazo zinaweza kumsaidia kuondoa majanga ya uhalifu kabla hayajatokea” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng’wilabuzu Ludigija amewataka watendaji wa kata kutumia taratibu za utawala bora katika kushughulikia migogoro ya kijamii.
“Leo tumepata elimu katika eneo la usalama lakini pia tumefundishwa ukamataji sahihi manayake tunapoenda kutekeleza majukumu haya tusiseme hilo halinihusu,” amesema Ludigija.
Naye Afisa kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Peter Dihoko anesema kiongozi mzuri ni yule anayehakikisha kuwa ana mifumo mizuri ya kupata taarifa na kushughulikia matukio kwa wakati.
“Kiongozi mzuri ni yule anayehakikisha mgeni yoyote anayeingia katika eneo lake la mamlaka anahakikisha anamtambua na anaweka mifumo mizuri ya kupata taarifa,” amesema Dihoko.