Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Kakozi Ibrahim amessma ni lazima mwelekeo wa uendeshaji wa Vyama vya Ushirika Nchini ubadilike, ili vijiendeshe Kibiashara, kuongeza tija, na kuchangia katika uchumi wa Taifa.
Kakozi ameyasema hayo hii leo Machi 28, 2025 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 30 wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU 1984 LTD ), uliofanyika katika ukumbi wa mikutano Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Amesema, Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) inasisitiza vyama vya ushirika kuwa na akaunti za benki katika benki ya Maendeleo ya ushirika, na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali kwa ajili ya kuboresha utendaji wa vyama hivyo.

“Tunataka kuona vyama vya ushirika vikijiendesha kibiashara, na sio tena kutegemea tu huduma za msingi. Vyama vya ushirika lazima viwe na nguvu na viwe na uwezo wa kufanya biashara ili kusaidia wanachama wao. Mapato yote yanayotokana na vyama vya ushirika ni mali ya umma , wanachama,” amesema Ibrahim.
Amesema vyama vya ushirika lazima viongeze nguvu katika kuzalisha mazao na kuwekeza katika miradi ya kiuchumi ili kuwa na michango inayokubalika.
Amehimiza kwamba wanachama wa vyama vya ushirika wasikubali kukaa na kulalamika, badala yake watumie rasilimali walizonazo kuboresha hali zao za kiuchumi.

“SHIRECU imekua kwa muda mrefu, lakini lazima tuondoke kwenye mazoea ya zamani ya kutoshughulika na mazao ya kilimo. Hatupaswi kukaa na kulalamika, tunazo rasilimali na nguvu za kufanya biashara kwa mafanikio,” amesema Mrajis Msaidizi huyo.
Akizungumzia ushirikiano na wadau, Ibrahim amesema vyama vya ushirika lazima vishirikiane na wadau wa kibiashara na wawe na mikakati ya kuzalisha bidhaa na huduma zitakazowawezesha wanachama kupata faida.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa vyama vya ushirika kushirikiana na wadau kama washirika na siyo kama wawekezaji.

“Nataka kuona viongozi na wanachama wanaoshirikiana na wengine kama washirika na siyo kama wawekezaji pekee. Vyama vya ushirika vinatakiwa kuwa na nguvu ya kufanya biashara na kuwa na misingi ya kujitegemea,” ameeleza Ibrahim.
Aidha, amesisitiza kuwa hakuna nafasi kwa viongozi au wanachama watakaokwama katika mabadiliko, akieleza kuwa kila mmoja lazima aonyeshe ufanisi katika kushughulika na mazao na kuwa na misingi imara ya kujitegemea.
“Muda wa kulalamika umekwisha. Vyama vya ushirika lazima viwe na mabadiliko ya kweli. Hatutavumilia kiongozi au mwanachama ambaye atasema ‘tumezoea hivi.’ Hatutaki kuona mtu akizuia maendeleo,” ameongeza.

Mkutano huo wa SHIRECU umelenga kuimarisha ushirika kwa kuhimiza mabadiliko ya kimfumo, kuanzisha mifumo ya kidijitali, na kuweka mikakati ya kibiashara ili kutoa manufaa kwa wanachama na jamii kwa ujumla.
Vyama vya ushirika vimetakiwa kuwa na umoja na kuwa na uwezo wa kufanya kazi kibiashara ili kuleta maendeleo endelevu.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo umejadili, kupokea na kuhuisha sera mbalimbali za Union, kujadili na kupitisha ukomo wa madeni, kupokea taarifa ya utekelezaji ya bodi ya SHIRECU na kupitisha mapendekezo ya bajeti kwa mwaka 2025/2026 ambayo ni shilingi bilioni 2.7 (Tsh. 2,729,477,473/=).
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa bodi ya chama hicho kwa niaba ya mwenyekiti wa bodi kaimu meneja mkuu wa SHIRECU mkoa wa Shinyanga Asnath Changamike amesema bodi hiyoimefanikiwa kukusanya mapato ya chama hicho kwa kukusanya faida tarajiwa Zaidi ya shilingi bilioni moja ambayo ni sawa na asilimia 68.61 ikiwa ni pamoja na kukusanya Zaidi ya shilingi milioni 97 yaliyokuwa madeni sugu.
Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga SHIRECU (1984) LTD kilisajiliwa tarehe 4 April, 1984 na kupewa Hati ya Usajili Namba 4123.Hata hivyo, kulingana na mabadiliko ya Mfumo wa uendeshaji wa Vyama vya Ushirika (MUVU) mnamo mwaka 2022, Chama kilifanikiwa kupata usajili mpya wenye namba AFF-SHY-SHY-MC-2022-9. Kwa sasa SHIRECU (1984) LTD inaundwa na Vyama vya Msingi 107 vinavyojishughulisha zaidi na zao la Pamba na mazao mengine mchanganyiko kwa maana ya Dengu na Choroko.


