NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA
Baadhi ya vyama vya upinzani mkoani Shinyanga,vimeeleza kuridhishwa na uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka huu,huku zikiomba dosari ndogondogo ambazo zilijitokeza, katika uchaguzi zifanyiwe kazi ili zisijitokeze kwenye uchaguzi mkuu uanotarajiwa kufanyika mwaka 2025.
Vyama hivyo ni CUF, Demokrasia Makini,NRA,CHAUMA pamoja na SAU.
Viongozi wa vyama hivyo wamebainisha hayo wakati wakizungumza na vyombo vya habari juu ya mwenendo na utoaji wa tathmini juu ya uchaguzi huo ambao umekamilika kwa chama cha mapinduzi (CCM) kuibuka na ushindi wa zaidi ya asilimia 90 huku vyama vingine vya siasa vikipata ushindi mdogo.
Wamesema uchaguzi huo umefanyika vizuri kwa amani na hapa kutokea vurugu zozote, isipokuwa uligubikwa na dosari ndogondogo,ikiwamo baadhi ya watu ambao sio waaminifu kuiba kura,pamoja na kukosekana majina kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura,na kuomba Uchaguzi Mkuu 2025 zisijitokeze dosari hizo.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa umma (CHAUMA) Mkoa wa Shinyanga Rashidi Katabanya, amesema uchaguzi umefanyika kwa amani na ulikuwa mzuri, isipokuwa hizo dosari ndogondogo, na kuiomba serikali katika uchaguzi mkuu mwakani (2025) ijipange vizuri ili uwe huru na haki.
Uchaguzi serikali za mitaa umekamilika hapa nchini ambapo uchaguzi huu ufanyika kila baada ya miaka mitano lengo likiwa ni kuimarisha uwakilishi katika maeneo husika pamoja na kuzipa jumuya za wananchi uwezo wa kufanya maamuzi yao mathalani matumizi ya ardhi ,miradi ya kijamii pamoja na utoaji wa huduma.