
Serikali ya Msumbiji imesema Vurugu zilizotokea ndani ya jela katika mji mkuu wa Msumbiji zimesababisha watu 33 kupoteza maisha na wengine 15 kujeruhiwa, huku zaidi ya wafungwa 1,500 wakitoroka.
Mkuu wa Polisi Msumbiji, Bernardino Rafael akizungumza Jumatano alisema wafungwa 150 waliokimbia gereza la Maputo wamekamatwa tena.
Wakati Rafael akilaumu maandamano nje ya gereza hilo kwa kuchochea vurugu hizo, Waziri wa Sheria, Helena Kida aliambia kituo cha televisheni cha kibinafsi cha Miramar TV kwamba machafuko hayo yalianzishwa ndani ya gereza hilo na hayana uhusiano wowote na maandamano nje.
“Makabiliano baada ya hapo yalisababisha vifo vya watu 33 na 15 kujeruhiwa karibu na jela,” Rafael aliambia mkutano na vyombo vya habari.
Ripoti ya Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) ilisema wafungwa hao waliwazidi nguvu walinzi na kukamata bunduki aina ya AK-47 na kuwaruhusu kutoroka Jela.
Mwandishi wa habari wa Msumbiji Clemente Carlos aliiambia SABC kuwa waliotoroka huenda walitumia fursa ya msimu wa likizo ya Krismasi, wakati walinzi wanaokua zamu wanakua wachache ikilinganishwa na siku za kawaida za kazi.
Taarifa ya Plataforma Decide inayohusika na ufatiliaji wa uchaguzi imesema idadi ya vifo nchini Msumbiji vimefikia 151 tangu Oktoba 21 2024.