Na Saulo Stephen – Singida.
Kamati ya Fedha na Utawala ya Manispaa ya Singida, imefanya ziara maalum ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na Halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha thamani ya fedha na ubora wa miradi vinazingatiwa.
Katika ziara hiyo, iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, JoanFeith Kataraia pamoja na Mstahiki meya wa manispaa hiyo Geoffrey Mdama,kamati imetembelea na kukagua ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Ng’aida, mradi unaotekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri kwa gharama ya shilingi milioni 239.
Aidha, kamati hiyo imekagua ujenzi wa shule mpya ya mkondo mmoja katika eneo la Unyamikumbi B unaotekelezwa chini ya mradi wa BOOST kwa gharama ya shilingi milioni 302.

Sambamba na hayo kamati pia imetembelea ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Zahanati ya Unyamikumbi, unaogharimu shilingi milioni 148 kutoka mapato ya ndani.
Katika hatua nyingine, kamati hiyo imekagua mradi wa ujenzi wa ofisi ya usimamizi wa mradi wa TACTIC, ambao umefikia asilimia 60 ya utekelezaji wake, ukiwa na thamani ya shilingi bilioni 1.6. Kamati ilisisitiza kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa.


