VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA MARA VYAAGIZWA KUTUMIA MFUMO WA GoTOMIS

Na Adam MsafiriMara

Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi,ameziagiza halmashauri zote tisa za mkoa huo kuhakikisha kuwa hadi kufikia Agosti 31,2025,mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji na ufuatiliaji wa taarifa za utekelezaji wa huduma za afya (GoTOMIS) uwe umefungwa na kuanza kutumika katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya mkoani humo.

Kanali Mtambi ametoa maagizo hayo Julai 25,2025 wakati akikabidhi kompyuta 142 na vifaa vingine vya kidigitali kwa vituo vya serikali vya kutolea huduma za afya,huku akiwasisitiza watumishi wa kada ya afya kuhakikisha wanavitumia vifaa hivyo kikamilifu ili kupandisha matumizi ya mifumo ya kidigitali na kufikia asilimia mia moja.

“Naagiza vituo vyote vya kutolea huduma za afya vihakikishe vinatumia mfumo huu wa GoTOMIS ifikapo tarehe 31 Agosti mwaka huu,sitarajii kwamba kwa kutmia mifumo hii kwenye zahanati zetu sasa kusiwe na kisingizio cha kuchelewesha huduma au huduma kutokutolewa kwa kiwango kitakiwacho kwa wananchi.”Amesema Kanali Mtambi.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa wa Mara amesema kuwa”Ni matumaini yangu sasa baada ya kutolewa kwa vifaa hivi matumizi ya kidigitali kwenye vituo vyetu vyote vya kutolea huduma za afya,yatapanda na kufikia asilimia 100 hatuna sababu yoyote ya kutofanya kazi kidigitali”.

Awali Katibu Tawala wa mkoa wa Mara Bw.Gerald Kusaya amebainisha kuwa kufungwa mifumo ya kidigitali ya mawasiliano na ufuatilia ya GoTOMIS kwenye vituo vya serikali vya kutolea huduma za afya,kutasaidia kudhibiti mapato ya serikali pamoja na kurahisisha mawasiliano kwa njia ya kidigitali.

“Kwa jinsi tunavyoendelea ni vyema haya mambo yakafanyika kimfumo zaidi,mfumo utasaidia katika suala la udhibiti wa mapato ya serikali lakini pia mifumo hii itaturahisishia katika suala la mawasiliano pamoja na kufuatilia hali ya utendaji kazi katika mkoa wetu”.Amesema Kusaya.

Nao baadhi ya watumishi wa kada ya afyawameiambia Tovuti hii kuwamfumo wa kidigitali wa GoTOMIS una manufaa makubwa katika utendaji huku wakitoa wito kwa watumishi wengine wa kada hiyo kuutumia mfumo huo bila kisingizio ili kufanikisha lengo la serikali la kuhakikisha taasisi zake zinaendeshwa kidigitali na kwa tija zaidi.

Mkoa wa Mara hadi sasa una jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya vipatavyo 324 huku ikielezwa kuwa matumizi ya utoaji huduma kwa wananchi kupitia mifumo ya kidigitali yamefikia asilimia 90,na kwamba serikali itaendelea kuwezesha taasisi zake kupata miundo mbinu na vifaa vya kidigitali ili kufikia asilimia 100 ya utoaji huduma kidigitali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *