Na Belinda Joseph – Songea.
Viongozi wa ngazi ya mashina zaidi ya 4,000 kutoka Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, wamepatiwa mafunzo maalum ya kisheria kwa muda wa siku tatu kuanzia Mei 10, 2025. Mafunzo haya yalifanyika katika ukumbi wa Kanisa la Anglikana uliopo Songea Mjini, yakihusisha mabalozi wa nyumba kumi, wajumbe wa mashina pamoja na watendaji wao.
Lengo kuu la mafunzo haya lilikuwa ni kuwawezesha viongozi hao kupata maarifa kuhusu masuala ya utawala bora, uraia, njia mbadala za kutatua migogoro, kupinga ukatili wa kijinsia, pamoja na elimu ya uchaguzi.

Waziri wa Katiba na Sheria, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, alifungua rasmi mafunzo hayo akiwa ameambatana na timu ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (Samia Legal Aid).
Akizungumza katika ufunguzi huo, Dkt. Ndumbaro alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipambanua katika kuboresha huduma za haki kwa wananchi, hatua ambayo inachochewa na ushirikiano mzuri kati ya wananchi na Serikali yao kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Waziri huyo aliongeza kuwa utolewaji wa msaada wa kisheria kwa wakazi wa Songea ni ishara ya kutambua ukarimu mkubwa waliouonesha kwa Mheshimiwa Rais wakati wa Tamasha la Sanaa na Utamaduni lililofanyika mkoani humo.
“Tamasha hilo limeongeza thamani ya mkoa wetu, na kwa hakika limetoa msukumo kwa Serikali kuimarisha huduma muhimu kwa wananchi kama vile miundombinu ya barabara, vituo vya afya na elimu,” alisema Dkt. Ndumbaro.

Akiwaaga washiriki wa mafunzo hayo, Ndumbaro aliwasihi wananchi wote waliojiandikisha kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kupiga kura. Alibainisha kuwa ushiriki huo ni njia ya kulinda misingi ya demokrasia na kuchochea maendeleo ya taifa.
Aidha, alisisitiza kuwa mafunzo haya ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuwajengea wananchi uwezo wa kuelewa haki na wajibu wao katika jamii wanazoishi.