VIONGOZI WA DINI, WAZEE WA KIMILA WAHIMIZWA KUELIMISHA MADHARA YA RUSHWA

Viongozi wa dini na Wazee wa kimila wametakiwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya rushwa, kwani mbali na kuwa ni kosa kisheria lakini pia ni kinyume na maadili ya kiimani.

Akizungumza katika Semina maalum iliyoandaliwa na TAKUKURU, Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego aliwahimiza Wananchi kushiriki kikamilifu katika kupambana na rushwa, hasa kipindi cha uchaguzi.

Amesema, Vongozi wa dini na Wazee wa kimila wanatakiwa kuendelea kuhamasisha uadilifu na uwajibikaji ndani ya jamii, ili kuepusha migongano, uvunjifu wa maadili na uminyaji haki unaotokana na vitendo vya rushwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Sifa Mwanjala amesema lengo la semina hiyo ni kuwawezesha viongozi wa dini, wazee wa kimila, na viongozi wa taasisi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.

Amesema, rushwa imekuwa ikikwamisha maendeleo kwa kusababisha miradi kutotekelezwa ipasavyo, hali inayowanyima Wananchi huduma muhimu walizostahili na kwamba pia huchochea vitendo vingine vya kihalifu ikiwemo wizi, unyanyasaji wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Nao baadhi ya Washiriki wa semina hiyo akiwemo Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Singida, Ally Ommary Nuna na mzee Joseph Sabole wamesema rushwa imekuwa inakihatarisha utulivu katika jamii na kukwamisha maendeleo.

Aidha, wamependekeza uwepo wa mwendelezo wa utoaji wa mafunzo kama haya kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama, ili kuwezesha uwekaji wa mikakati madhubuti ya kupambana na rushwa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *