VIONGOZI WA DINI WAOMBWA KULIOMBEA AMANI TAIFA LETU….

Na SAADA ALMASI – SIMIYU

Wakati Taifa likijiandaa na uchaguzi mkuu hapo mwezi Octoba mwaka huu viongozi wa dini wameombwa kuendelea kuliombea amani na kulikabidhi kwa Mungu ili zoezi hilo lifanyike katika hali ya utulivu. Rai hiyo imetolewa na Shauli Machungwa katibu wa mlezi wa wafugaji Tanzania Joseph Makongolo alipokuwa akikabidhi baiskeli kutoka kwa mlezi huyo kwa viongozi wa dini katika kata ya Ligangabilili wilayani Itilima mkoani Simiyu.

Machungwa amesema kuwa viongozi wa dini ndio wanaobeba maono ya nchi na kupitia baiskeli hizo  zitawarahisishia kupita maeneo yaliyokuwa changamoto kwao huku wakihubiri amani na kufanya maombi ya kuwajenga watu kiimani  na hatimaye kuliokoa taifa.

“Mnakusanya watu wa aina mbalimbali na pale mnapowahubiri neno la Mungu mnabadili mioyo yao kwa amri zake,mlikuwa na changamoto ya usafiri sasa kaendeleeni kufanya maombi muwafikie wengi zaidi ili amani idumu na muwaase wakachague viongozi ambao watawatetea na si kuleta mfataruku baina yao” – katibu Machungwa.

Akipokea baiskeli hizo Askofu wa kanisa la Sore Evangelist Church wilaya ya Itilima Burton Mashishanga amesema kuwa huduma za kiroho ndio silaha pekee itakayomjenga mtu yoyote katika kufanya maamuzi sahihi hivyo watahakikisha wanakutana na waamini katika maeneo yote ili wamjue Mungu na watende mema kulingana na mafundisho.

“Tutafika hata pale ambapo ilikuwa kazi kufika ili watu wote wamjue Mungu,watambue kusudi lake na hatimaye wafanye machaguo sahihi ili amani iendelee nchini” – Askofu Mashishanga.

Kwa upande wake sheikh wa kata ya Munze Rashid Abbas ambaye anahudumia zaidi ya waamini 400 kutoka vijiji vya Madilama,Mhunze ,Majulesi na Dusara ambavyo vina changamoto ya kufikika kwa usafiri tofauti na baiskeli amesema kuwa kwa sasa kazi yake inakwenda kuwa rahisi na kwamba ataendelea kuhubiri amani ili nchi ibaki salama.

“Kuna maeneo tunafika baada ya kupita katika majaluba ya mpunga ambapo pikipiki inakwama haiwezi kupita lakini ukiwa na baiskeli unaweza ukaibeba ukavuka kisha ukaendelea na safari,lakini pia zipo nchi nyingi ambazo hazina amani hivyo tunaamini sasa kazi ya kueneza elimu ya dini na amani kwa ujumla itakuwa rahisi” – Sheikh Rashid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *