VIONGOZI WA DINI KIGOMA WAPEWA ELIMU MASUALA YA RUSHWA

Na Faustine Kasala – Kigoma.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Kigoma, imeendesha mafunzo kwa Viongozi wa Dini Manispaa ya Kigoma Ujiji, ili kuwajengea uelewa wa masuala ya Rushwa.

Akifungua Mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika katika Ofisi za Taasisi hiyo Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, Asha Kwariko amesema katika kipindi hiki cha uchaguzi  wamekuwa wakipokea taarifa za uwepo wa Rushwa zinazofanywa na baadhi ya wagombea kupitia nyumba za ibada.

“Tunazo taarifa baadhi yenu  mnatumika na wanasiasa, mnawapa majukwaa hukohuko katika nyumba za Ibada mnapokea pesa na kuwaelekeza waumini wenu cha kufanya, sasa tumewaita ili kuwakumbusha wajibu wenu kabla hatujawafikia,” alisema Asha.

Amesema, Jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa ni la kila mmoja hivyo jamii inapaswa kushiriki kikamilifu katika utoaji wa taarifa za Rushwa hususani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu 2025.

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Elimu kwa umma TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, Ibrahim Sadiki amesema athari za rushwa ni pamoja na kukosekana kwa haki katika jamii, udhalilishaji wa utu wa mtu kwa kulinganishwa na thamani ya utu na Rushwa anayopewa mtu huyo

“Ndugu zangu naomba mfahamu vitendo vya Rushwa hususani katika chaguzi za Kisiasa vinaathiri  mchakato mzima  wa Demokrasia ya uwakilishi na maendeleo ya Taifa, nawaombeni sana msijiingize huko na muendelee kuwakemea waamini wenu ili nao wajiepushe na masuala ya Rushwa,” alisema Ibrahim.

Kwa upande wake Mhubiri wa Madhehebu ya Kiislamu Halmashauri ya wilaya ya Kigoma Swalehe Issa Nzwiba amesema Viongozi wa Dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini wanapaswa kujitafakari hususani wale ambao wamekuwa wakiruhusu madhabahu zao kutumika na wanasiasa kupenyeza ajenda zao za kisiasa.

“Ni kweli hatuwezi kujitenga na siasa lakini inakuwa mbaya zaidi pale ambapo mchungaji au Shekhe anapokea pesa za mwana siasa kwa mlengo wa Rushwa ili kuwaelekeza waumini wake chakufanya kwa mgombea inatutia doa katika Taasisi zetu,” alisema Swalehe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *