Serikali Wilayani Musoma mkoani Mara, imeanza misako maalumu dhidi ya vikundi zaidi ya 600 vilivyokopa mikopo ya asilimia 10 na kushindwa kurejesha fedha hizo katika Manispaa ya Musoma.
Hatua hiyo, inachukuliwa ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha uwajibikaji kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, vinavyonufaika na mpango wa mikopo ya asilimia 10.

Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi ya shilingi milioni 89, kwa ajili ya vikundi hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema tayari ameunda kikosi kazi kinachojumuisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kuwabaini wadaiwa sugu na kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa.
Amesema, fedha hizo ni za umma na zinapaswa kurejeshwa kwa wakati ili ziweze kuwanufaisha wananchi wengine wanaohitaji mikopo hiyo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

“Yeyote yule aliyechukua fedha za mkopo wa asilimia 10 katika Manispaa hii arudishe kwa haraka,kwa sababu hatutomuonea haya yeyote tunakwenda kuchukua hatua kali za kisheria.” Amesema Chikoka.
Kwa upande wao uongozi wa Manispaa ya Musoma umetaja changamoto ya baadhi ya vikundi kukopa mikopo bila kuiwekeza kwenye shughuli za uzalishaji, hali inayosababisha kushindwa kurejesha fedha kwa wakati uliopangwa huku naye Mbunge wa Musoma mjini Mgore Miraji akiiomba serikali kuwashughulikia ipasavyo wale wote walioshindwa kurejesha mikopo hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya wanavikundi walionufaika na mikopo hiyo wamesema, wapo tayari kushirikiana na serikali kwa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanarejesha fedha walizokopa kwa wakati.
Kwa mujibu wa taarifa za Manispaa ya Musoma, jumla ya mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia mbili tayari imeshatolewa kupitia mpango wa asilimia kumi kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.