VIKUNDI 55 SINGIDA VYAPATIWA MKOPO WA MILIONI 820

Na Saulo Stephen – Singida.

Jumla ya vikundi 55 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida, wamepatiwa mkopo wa asilimia 10 utokanao na mapato ya ndani kiasi cha Shilingi milioni 820 kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi kupitia Biashara mbalimbali.

Mkopo huo umetolewa mbele ya Mgeni rasmi ambae ni Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Bi Anna Makinda,kwenye kongomano lililoandaliwa kwa lengo la kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan lililofanyika Juni 20,2025 kwenye ukumbi wa kanisa la Waadiventista Wasabato uliopo Ititi Mkoani Singida.

Miongoni mwa Vikundi vilivyonufaika na Mkopo huo wa awamu ya tatu ya utoaji mkopo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 vikundi 40 ni vya wanawake, Vikundi 13 vya vijana na Vikundi viwili vya watu wenye ulemavu.

Wakizungumza mara baada ya kupokea mkopo huo baadhi ya wawakilishi wa vikundi hivyo vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu wamemshukuru uongozi wa manispaa ya Singida pamoja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mkopo huo.

Wanasema wanaamini utakwenda kuwasaidia katika Biashara zao na kujikwamua kiuchumi huku wakiahidi kurejesha mkopo huo kwa wakati ili na vikundi vingine viweze kunufaika na mkopo huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *