VIJANA WACHUKUE MIKOPO KWA MALENGO KUBADILISHA MAISHA – WANA IKOLA

Wananchi wa Kata ya Ikola, Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi wameeleza furaha yao kwa kupata mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu huku wakitoa rai kwa Vijana kuchukua mikopo kwa malengo yatakayobadilisha maisha yao kwa manufaa chanya.

Kwa kuwa eneo lao lipo mwambao wa Ziwa Tanganyika, wananchi hao wameona fursa ya kipekee ya kutumia rasilimali za Ziwa hilo katika kujipatia kipato ikiwemo Uvuvi na Biashara ya Dagaa na Samaki.

Wanasema, kabla ya mikopo hiyo walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya mitaji midogo, lakini sasa wameweza kuongeza uwekezaji na kujipatia maendeleo zaidi ya kiuchumi.

Aidha, wametoa rai kwa Vijana na Wananchi wenzao kiujumla, kutumia fursa ya mikopo ya Halmashauri kwa ubunifu na kufanya biashara zitakazowawezesha kujikwamua kimaisha.

Kwa upande wa Serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Reginald Clavery amesema kuwa kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2024/2025 walitoa fedha kwa vikundi mbalimbali na kubaki na zaidi ya shilingi milioni 251 zitakazotolewa kwa wananchi katika katika awamu ya pili.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, wamewataka wananchi kufuata utaratibu sahihi wa kuunda vikundi na kuomba mikopo, huku akisisitiza kwamba rasilimali hizo zipo kwa ajili ya kila mmoja, ili mradi azingatie masharti.

Kwa sasa, maafisa maendeleo ya jamii wametakiwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi wote, ili mikopo hii iwe chachu ya maendeleo ya kweli katika mwambao wa Ziwa Tanganyika na Halmashauri kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *