
Wananchi wa Kata ya Chambo halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga Wametakiwa kudumisha amani na utulivu ikiwa ni Pamoja na kuwasihi vijana kujiunga na jeshi la Sungusungu ili kuimarisha Ulinzi katika vitongoji vyao.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga na mjumbe wa kamati ya Siasa mkoa Ndg. Simoni Mayengo wakati akiongea na wananchi wa Kitongoji cha Ntungulu katika Kijiji cha Nyawishi.
“Ndugu zangu swala la ulinzi na usalama wa vitongoji vyetu utaletwa na sisi wenyee,sasa niwaombe vijana wajitokeze kujiunga na jeshi la sungusungu ili kudumisha ulinzi katika kitongoji chetu” Amesema Mayengo.
Sambamba na hayo Mayengo amesema kuwa kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu za mwisho wa mwaka kumekuwa na matukio Mengi ya Uhalifu ambayo mengine yanapelekea mauaji na kuwataka wananchi kuunda vikundi vya ulinzi katika kila kitongoji ili kuwa na umoja katika Ulinzi Shirikishi.

“Sikukuu zimekaribia niwaombe sasa undeni vikundi ili kukomesha haya matukio na muwe na mawasilino baina ya kitongoji kimoja na kingine ili kuungana katika ulinzi”.Ameongeza Mayengo
Katika hatua nyingine Mayengo amesema kuwa Watu wanaofanya matukio ya Uhalifu na uhalifu hawatoki mbali na kwamba mtu anayefahamu watu wanaofanya uhalifu wowote watoe taarifa za Siri kwa viongozi wa Sungusungu au Polisi kata ili waweze kuzifanyia kazi taarifa hizo.
“Toeni taarifa za siri za waharifu ili jeshi la polisi lifuatilie matukio haya,Na taarifa hizi ni za siri hakuna mtu atakayetajwa kuwa ndo katoa taarifa” Amesisitiza Mayengo.
Nao baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Ntungulu wamemshukuru Ndugu Simoni Mayengo kwa kuwapa elimu ya Ulinzi Shirikishi na kutoa wito kwa wazazi na Walezi kuwaruhusu vijana kujiunga na jeshi la Sungusungu ili kuimarisha ulinzi katika kitongoji Chao.
“Kwakweli tunamshukuru Sana Mjumbe wa chama kwa ushauri huu,Hakika tumemuelewa sana kuhusu ulinzi shirikishi na sasa tuwaombe wazazi wawaruhusu vijana wao kujiunga na sungusungu ili ulinzi wetu uimarike” Alisema mmoja wa walinzi wa jadi Bwana Mussa Athuman.