Na Tryphone Odacee, Kasulu – Kigoma.
Baadhi ya Vijana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma wameanza kunufaika na fursa za kiuchumi kupitia ubunifu wa nishati safi, kufuatia kuanzishwa kwa kiwanda cha uzalishaji wa mkaa mbadala katika Kata ya Rusesa.
Kiwanda hicho kimeanzishwa na taasisi ya Disability Relief Services Tanzania (DRST) kupitia kituo cha vijana kinachojulikana kama Youth Hub, kwa lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia ubunifu wa kijani, matumizi ya nishati safi na utunzaji wa mazingira.

Akizungumza wakati wa maonesho ya vibanda yaliyoandaliwa na DRST katika viwanja vya Kijiji vya Rusesa, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Elikana Maige, aliipongeza DRST kwa kuanzisha mradi huo.
Maige alisema matumizi ya nishati safi yana umuhimu mkubwa katika kupunguza uharibifu wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha aliwahimiza vijana kutumia fursa zinazotokana na ubunifu wa kijani ili kujiajiri, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira.
Mkurugenzi wa DRST, Jeremiah Mutagoma, alisema shirika hilo hadi sasa limewafikia wananchi katika kata nane kupitia shughuli mbalimbali za kuwawezesha wananchi na vijana.

“Naomba ushirikiano kati ya DRST na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ili tuendelee kuimarika, ili kuwezesha shirika hili kuwafikia vijana wengi zaidi, hususan katika kata ambazo bado hazijafikiwa na programu hizi” alisema Mutagoma.
Kwa upande wake, Kelvin Kimaro kutoka Divisheni ya Maendeleo ya Jamii ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, aliwahimiza vijana kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya Halmashauri hiyo akitaja miongoni mwa fursa hizo kuwa ni mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi maalum, ambayo inaweza kuwasaidia vijana kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, Mary Zilandise, mmoja wa wanufaika, alisema kiwanda hicho kimekuwa chanzo cha ajira kwa vijana huku akioa shukrani kwa Serikali na DRST kwa kuwawezesha vijana kupata fursa za kiuchumi kupitia mradi huo wa nishati safi.
“Mradi huu umetupatia ajira na kutuwezesha vijana kupata fursa za kujikwamua kiuchumi” alisema Zilandise.

Mradi wa uzalishaji wa mkaa mbadala ni miongoni mwa jitihada zinazolenga kuwashirikisha vijana katika shughuli za kiuchumi zinazozingatia uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi.


