VIJANA 102 WAPEWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KIGOMA

Na Tryphone Odace – Kigoma.

Jumla ya Vijana 102 kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma, wamepatiwa mafunzo ya ujuzi mbalimbali, huku wakitakiwa kujikita katika ujasiriamali utakaowawezesha kujipatia kipato badala ya kusubiri ajira.

Mafunzo hayo, yametolewa kwa vijana na Shirika la Women Promotion Center ambayo yanalenga kuwainua vijana, ili waweze kujitegemea kwa kufanya kazi mbalimbali zitakazowapatia kipato, ikiwemo ushonaji, ujasiriamali na kuwajengea uwezo wa kujiamini, ili wanapokutana na vikwazo waweze kuvikabili.

Naye Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Lucia Mayuma kutoka shirika hiyo amesema katika mafunzo hayo yamelenga kuwafundisha vijana, ili waweze kujaribu na kuthubutu kufanya jambo ambalo linaweza kumpa nafasi ya kupata pesa na kuaminika kwenye jamii na namna ya kuendesha bidhaa wanazokuwa nazo.

“tumewafundisha mambo mengi ambayo tunaamini yatawasaidia kuweza kufika mbali kikubwa ni wao kuwa wavumilivu na baadhi ya masomo tumewapa ujuzi wa namna ya kuanzisha biashara hata kama ni ndogo lakini itakuwa vizuri iwapo itakuwa imepata usimamizi bora,” amesema Mayuma.

Naye Mkurugenzi wa shirika la Women Promotion Center, Matha Jerome, amewataka vijana kuamka na kufanya kazi kwa bidii badala ya kusubiri kuajiriwa, akisisitiza kuwa uvivu ni miongoni mwa sababu zinazochangia umasikini kwa vijana kwani waliowengi huogopa kujaribu hali inayosababisha kuingia kwenye vitendo viovu.

“Vijana wa siku hizi wanapenda mafanikio ya haraka bila kujua kuwa mafanikio hayawezi kuja bila kufanya kazi ambazo zitakusaidia kupata pesa” amesema Jerome.

Kwa pande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kasimbu, Deograsias Tanda amesema serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya vijana kupitia mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri kupitia mapato ya ndani na hivyo hawana budi kutumia mikopo hiyo kujiajiri kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

“Halmashauri kila mwaka inatenga mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa hiyo mnayo nafasi ya kupata mitaji na mkaendeleza ujuzi mnaokuwa mmepata hapa baada ya kuomba mikopo hiyo kupitia vikundi” amesema Tanda.

Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2025 Shirika la Women Promotion Center liliwezesha vikundi vya vijana takribani 64 vilivyojikita katika shughuli mbalimbali za biashara na machi 9, 2026, shirika hilo liliwezesha mashine za cherehani 114 kwa vikundi 38, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *