VIGOGO WA SOKA TZ WAZIJUA TIMU PINZANI MASHINDANO KIMATAIFA

Vigogo wa soka Nchini Tanzania, wamewafahamu wapinzani wao katika michuano ya Kimataifa, ambapo Yanga SC wamepangwa kucheza dhidi ya Gaborone Utd ya Botswana kwenye hatua ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wananchi wataanzia ugenini kwenye mechi itakayopigwa kati ya Septemba 4 hadi 6, 2026 na kurudiana nyumbani kati ya Septemba 11 hadi 13, 2026.

Wekundu wa Msimbazi Simba SC, wao wataanzia hatua ya awali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2026/27 kwa kuvaana na Mighty Wanderers ya Malawi.

Mnyama ataanzia ugenini kati ya Septemba 16 hadi 18, na mchezo wa marudiano utapigwa kati ya Septemba 23 hadi 25, 2026.

Wakati huo huo, wawakilishi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), Azam FC wenyewe watakutana na mmoja kati ya Djibouti Télécom ya Djibouti na ZED FC ya Misri kwenye raundi ya pili ya awali ya baada ya droo ya CAFCC iliyoganyika leo.

Djibouti Télécom ya Djibouti na ZED FC ya Misri zitachuana kwenye hatua ya awali ambapo mshindi wa matokeo ya jumla atakata tiketi ya raundi ya pili ya awali kabla ya kukutana na Azam FC.

Nao wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye CAFCC, Singida Black Stars wamepangwa dhidi ya Al Ghazala SC kwenye raundi ya kwanza ya hatua ya awali.

Mshindi wa matokeo ya jumla atachuana na mmoja kati ya Al Ahly FC ya Sudan au Tusker FC ya Kenya kwenye raundi ya pili ya hatua ya awali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *