Vifo vya mama wajawazito vyapungua nchini

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete ameipongeza Serikali kwa kufanikiwa kupunguza vifo vya akinamama wajawazito kutoka vifo 556 556 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 104 mwaka 2022.

Dkt. Kikwete amesema hayo wakati akifungua kongamano la pili la kisayansi la afya ya uzazi mama na mtoto ambalo linafanyika jijini Dar Es Salaam linalojumuisha wataalam mbalimbali wa sekta ya afya.

Dkt. Kikwete amesema mwaka 2000 hadi 2015 katika malengo ya Milenia yalitaka nchi zinazoendelea kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kufikia 191 kwa kila vizazi hai laki moja, lakini Tanzania mwaka 2015 tulifikia vifo 432 katika vizazi hai laki moja na vikaendelea kuongezeka hadi kufikia 556 mwaka 2016.

“Mwelekeo wa sasa wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni mzuri, vifo vimepungua kutoka 556 mwaka 2016 hadi kufikia 104. Hii ni hatua kubwa naipongeza Serikali na Wizara ya Afya kwa jitihada ilizoweka. Ni jambo la kufedhehesha kuona mama ambaye analeta uhai wa kiumbe duniani anapoteza maisha”. Amesema Jakaya Kikwete.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuru Dkt. Kikwete katika awamu yake ya uongozi kwa kutambua na kuthamini huduma za afya ya uzazi ambapo mwaka 2014 alizindua mpango wa kuchochea huduma bora za afya ya uzazi ili kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na Watoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *