Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameielekeza Kamati inayoshughulikia Masuala ya Mashariki ya Kati ya Umoja huo kutembelea eneo hilo mapema katika juhudi za kutafuta suluhusho linaloweza kuhakikisha amani na usalama vinapatikana kufuatia mgogoro unaoendelea baina ya Israel na Palestina.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 30 Novemba, 2023 Jijini Tel Aviv nchini Israel mara baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya siku mbili iliyompa fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Viongozi mbalimbali wa Israel.
Amefafanua kuwa, moja ya msingi wa IPU ni kuhakikisha uhai wa kila binadamu unalindwa na Umoja huo utafanya kila linalowezekana ili dunia iwe sehemu salama na ya amani kwa binadamu wote bila kujali rangi, itikadi, imani na maeneo wanayotoka. Aidha amesisitiza kuwa, Mpango mkakati wa Umoja huo ni kuutumia Mwaka 2024 pamoja na mambo mengine kujadili kwa kina suala la Amani na Usalama kama ajenda muhimu kwenye Mikutano yake Mikuu ya mwezi Machi na Oktoba 2024.


