Katika hali isiyokuwa ya kawaida mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Bugumba Misalaba Mkazi wa Mtaa wa Nyakato kata ya Nyanguku wilaya na Mkoa wa Geita ameonekana akiwa hai baada ya kufariki kwa ajali ya Gari Novemba 15 2020.
Wakizungumza na Jambo FM baada ya kufika eneo la tukio, baadhi ya ndugu wa mwanamke huyo wamesema Bugumba Misalaba alifariki kwa ajali ya Gari wilayani sengerema Mkoani Mwanza toka Novemba 2020 na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti ambapo baadaye ndugu walikwenda na kuutambua mwili na kuzika.
Pia baadhi ya wakazi wa mtaa huo wamesema baada ya familia kutoa taarifa za kifo cha mwanamke huyo walishiriki kuuaga mwili na kumzika.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Mkuu wa wilaya ya Geita Cornel Magembe amesema mtu huyo alifariki kwa kugongwa na Gari wakati akiendesha Baiskeli kutoka wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza hali iliyopelekea kifo chake na baada ya kuonekana tena akiwa hai ndugu zake wamejiridhisha kuwa ni yeye na amewataka ndugu pamoja na wananchi kuwa watulivu wakati jeshi la polisi linafanya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.